Skip to content

Manuel Neuer ajitetea baada ya Ujerumani kupoteza dhidi ya Ecuador

SokaNews
Updated: Published: Ijumaa, 26 Juni 2026 · 2 min read
manuelneuer ujerumani ecuador kombeladunia juliannagelsmann
Manuel Neuer ajitetea baada ya Ujerumani kupoteza dhidi ya Ecuador

Neuer ajibu mapigo kuhusu lawama za bao la ushindi

Kipa namba moja wa timu ya taifa ya Ujerumani, Manuel Neuer, amejikuta katika mvutano na waandishi wa habari baada ya timu yake kupokea kipigo cha kushtukiza kutoka kwa Ecuador katika mchezo wa Kundi E. Ujerumani ilijikuta ikipoteza mchezo huo kwa mabao 2-1, matokeo yaliyoiwezesha Ecuador kufuzu hatua ya 32 bora.

Katika mchezo huo, Ujerumani ilianza kwa kasi kwa bao la mapema la Leroy Sane, lakini Ecuador walirudisha bao kupitia kwa Nilson Angulo kabla ya Gonzalo Plata kufunga bao la ushindi dakika za lala salama. Bao la Plata lilitokana na makosa ya kiufundi ambapo Neuer alijaribu kuudaka mpira uliokuwa ukielekea langoni, lakini mshambuliaji huyo alikuwa mwepesi na kuuwahi mpira huo kabla ya kipa huyo.

”Siwezi kuyeyuka uwanjani”

Baada ya mchezo kumalizika, baadhi ya wachambuzi na waandishi walimnyooshea kidole Neuer wakidai alifanya makosa katika nafasi aliyochukua kabla ya bao hilo. Kipa huyo wa Bayern Munich hakukubaliana na tuhuma hizo, akisisitiza kuwa hatua alizochukua zilikuwa za kawaida kwa kipa yeyote.

“Ni mpira wa kawaida wa kichwa, na mimi nilikuwa najaribu kuudaka. Ni hali ya kawaida kabisa. Kipa yeyote ambaye amewahi kucheza anajua kuwa lazima nijiweke katika nafasi hiyo ili kuudaka mpira. Ilionekana kama bahati mbaya kwa sababu nilikuwa pale, lakini haikuwa kosa langu,” alisema Neuer.

Alipobanwa zaidi na mwandishi mmoja aliyedai kuwa kitendo kile kilionekana kuwa cha ajabu, Neuer alijibu kwa jazba:

“Sasa natakiwa kusimama vipi? Unataka nidie wakati mpira unakuja moja kwa moja kwangu? Lazima nisongee kuelekea kwenye mpira ili niudake. Ikiwa mtu ataweka mguu na mpira ukanipita, basi umenipita. Lakini siwezi tu kuyeyuka uwanjani (I can’t just evaporate),” aliongeza kipa huyo.

Nagelsmann akataa nadharia ya “kutokujituma”

Baada ya mchezo, baadhi ya wachezaji wa Ujerumani walidai kuwa Ecuador walistahili ushindi kwa sababu “walitaka ushindi zaidi” kuliko wao. Hata hivyo, kocha mkuu wa Ujerumani, Julian Nagelsmann, ameyaita madai hayo kuwa ni upuuzi mtupu.

Nagelsmann alionyesha kukerwa na mtazamo huo akisema:

“Ecuador walitaka ushindi zaidi kuliko sisi? Huo ni upuuzi. Tafadhalini acheni huu upuuzi. Je, vijana hawakutoa kila kitu leo? Walichukua hatari zaidi kwenye matukio mengi, lakini siwezi kusema kuna mchezaji yeyote ambaye hakutoa kila alichokuwa nacho uwanjani. Hiyo ni hoja rahisi sana kwangu,” alisisitiza kocha huyo.