Martin Zubimendi ataka kuondoka Arsenal, Real Madrid watajwa
Hatima ya Zubimendi Emirates mashakani
Kiungo wa klabu ya Arsenal, Martin Zubimendi, anatajwa kuwa na mpango wa kuondoka ndani ya klabu hiyo baada ya kupoteza nafasi yake ya kudumu katika kikosi cha kwanza. Taarifa kutoka nchini Hispania zimeeleza kuwa nyota huyo raia wa Hispania ameiweka Real Madrid kama chaguo lake namba moja endapo atafanikiwa kuondoka.
Zubimendi alijiunga na The Gunners katika dirisha la usajili la majira ya joto mwaka 2025 kwa ada iliyokadiriwa kufikia paundi milioni 60 akitokea Real Sociedad. Licha ya kuanza maisha ya London Kaskazini vizuri, kiwango chake kilibadilika kuelekea mwisho wa msimu uliopita na kupoteza nafasi yake kwa chipukizi Myles Lewis-Skelly.
Ujio wa Bruno Guimaraes wambana Zubimendi
Hali imekuwa ngumu zaidi kwa Zubimendi kufuatia hatua ya Arsenal kumsajili kiungo Bruno Guimaraes, jambo lililoongeza ushindani wa namba kwenye safu ya kiungo. Katika michezo ya hivi karibuni kabla ya mapumziko ya kimataifa, Zubimendi amekuwa akisota benchi na kushindwa kupata nafasi ya kuanza kwenye michezo ya Ligi Kuu ya England.
Ripoti zinaeleza kuwa kiungo huyo amewataka wawakilishi wake kuharakisha mazungumzo na mabingwa hao wa Ulaya, Real Madrid, ili aweze kurudi kwenye kiwango chake bora. Inaaminika kuwa Zubimendi anataka klabu itakayompa nafasi ya kuonyesha uwezo wake wa kuchezesha timu kutoka nyuma.
Arsenal wataja dau la kumwachia
Ingawa Arsenal hawataki kumuachia kiungo huyo kwa urahisi kutokana na kiasi kikubwa cha fedha walichokitumia kumsajili, wameonekana tayari kusikiliza ofa nzuri. Inaelezwa kuwa ofa itakayofikia Euro milioni 75 ikijumuisha ada ya awali na nyongeza nyingine, inaweza kuwashawishi mabosi wa Emirates kukubali dili hilo.
“Arsenal hawatamfanya kuwa rahisi kuondoka baada ya uwekezaji mkubwa walioufanya, lakini ofa ya Euro milioni 75 inaweza kubadili msimamo wao. Real Madrid wanafahamu hamu ya mchezaji ya kuondoka na wanajua hilo linaweza kuwa na faida kwenye mazungumzo magumu.”
Kwa sasa, Zubimendi anaonekana kutaka suluhu ya haraka ya hatima yake ya soka. Ingawa dirisha la Januari linaonekana kuwa muda mwafaka kwake kuondoka, klabu hizo zinaweza kusubiri hadi msimu wa joto wa 2027 ikiwa hazitafikia muafaka wa haraka wa kibiashara.