Michael Carrick 'anatelekezwa' na uongozi wa Man Utd, kibarua chake mashakani
Presha kwa Carrick na lawama kwa uongozi
Hali ndani ya Manchester United inazidi kuwa tete kwa kocha Michael Carrick. Timu hiyo imekuwa na matokeo duni msimu huu, ikishinda mchezo mmoja tu kati ya mitano ya mwisho katika mashindano yote, jambo ambalo limeanza kuibua maswali mazito kuhusu hatima yake ndani ya Old Trafford.
Licha ya presha hiyo, Mick Brown, aliyewahi kuwa mchambuzi mkuu na msaidizi wa meneja katika klabu hiyo, amesema kuwa Carrick anapaswa kupewa nafasi kwa sababu hapewi sapoti inayostahili na bodi ya klabu hiyo chini ya umiliki wa INEOS.
“Kuna presha kubwa kwa Michael Carrick kuleta matokeo. Hawajawa vizuri msimu huu, lakini hawezi kubeba lawama peke yake kwa sababu uongozi umeshindwa kumpa sapoti anayohitaji,” alisema Brown.
Mapungufu kwenye usajili na kikosi
Brown anasisitiza kuwa Carrick anafanya kazi na kile alichonacho, huku akionyesha kuwa uongozi wa United ulishindwa kufanyia kazi udhaifu wa wazi wa kikosi chao wakati wa dirisha la usajili. Klabu ilifanikiwa kuwasajili Andrey Santos, Youri Tielemans, na Carlos Baleba ili kuimarisha kiungo, lakini walikosa beki wa kushoto wa kusaidiana na Luke Shaw, pamoja na mshambuliaji wa kumrithi Joshua Zirkzee.
Uongozi pia umekosolewa kwa kugoma kutoa ada kubwa ya uhamisho ili kupata wachezaji waliolengwa kama Elliot Anderson na Mateus Fernandes, jambo ambalo limefanya kikosi hicho kukosa muunganiko uwanjani.
Mabadiliko katika benchi la ufundi
Wakati mjadala kuhusu nafasi ya Carrick ukiendelea, klabu imethibitisha kumuajiri Connor King kama kocha msaidizi wa makipa wa timu ya kwanza. King anajiunga na klabu hiyo akitokea Burnley, ambapo amekuwa akifanya kazi katika nyadhifa mbalimbali za ukocha tangu 2018.
King atafanya kazi chini ya kocha mkuu wa makipa, Craig Mawson, katika jitihada za kuboresha benchi la ufundi la Carrick. Hata hivyo, wengi wanaamini kuwa tatizo la United ni kubwa kuliko mabadiliko ya makocha wa kipa, huku majina kama Antonio Conte na Eddie Howe yakitajwa kama warithi wa Carrick iwapo ataamua kuondoka au kufutwa kazi.