Michael Olise aonyesha nia ya kujiunga na Real Madrid
Nia ya Olise kutua Santiago Bernabeu
Kiungo mshambuliaji matata wa Bayern Munich, Michael Olise, ameelekeza nia yake ya kutaka kujiunga na mabingwa wa Uhispania, Real Madrid. Mchezaji huyu wa kimataifa wa Ufaransa anaonekana kuamini kuwa Santiago Bernabeu ndio sehemu sahihi zaidi kwa ajili ya kuendeleza kiwango chake cha juu cha soka.
Tangu ajiunge na Bayern Munich akitokea Crystal Palace, Olise amekuwa na kiwango bora sana ambacho kimevutia macho ya klabu nyingi kubwa barani Ulaya. Takwimu zake zinaongea yenyewe, akiwa amehusika katika mabao 96 (magoli 42 na asisti 54) katika michezo 107 aliyoichezea klabu hiyo ya Ujerumani.
Real Madrid wanapanga rekodi
Habari kutoka kwa mwandishi Santi Aouna zinaeleza kuwa Real Madrid wako tayari kufanya kila liwezekanalo ili kumsajili nyota huyu. Inaaminika klabu hiyo ya jijini Madrid inataka kukamilisha dili hilo kwa rekodi ya uhamisho ili kuhakikisha wanampata mchezaji huyo ambaye anaonekana kuwa ‘Galactico’ inayofuata.
“Michael Olise anataka kujiunga na Real Madrid msimu huu wa joto. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa anaamini kuwa hiyo ndiyo klabu kamilifu kwa ajili ya kuendeleza maendeleo yake,” alieleza Aouna kupitia mtandao wa X.
Msimamo wa Bayern Munich
Licha ya presha kubwa kutoka kwa Real Madrid, msimamo rasmi wa Bayern Munich bado ni kwamba mchezaji huyo hauzwi. Hata hivyo, hali halisi inaonekana kuwa na utofauti kidogo. Inaelezwa kuwa klabu hiyo ya Bavaria inataka kumuongezea mkataba mpya wenye thamani kubwa, lakini pia wameanza kufanya mawasiliano na wachezaji wengine ambao wanaweza kuziba pengo lake endapo dili hilo litafanikiwa.
Fabrizio Romano, mtaalamu wa masuala ya usajili, amethibitisha kuwa Olise ni mchezaji anayemvutia sana rais wa Real Madrid, Florentino Perez.
“Jina la Mfaransa huyo limekuwa likitajwa katika mikutano ya Real Madrid mara kwa mara. Olise bado ni ndoto ya Real Madrid,” aliongeza Romano.
Kwa sasa, Olise anatarajiwa kufanya mazungumzo na uongozi wa Bayern Munich mara tu baada ya majukumu yake ya michuano ya Kombe la Dunia kumalizika. Mashabiki wengi wa soka wanaisubiri kwa hamu hatima ya mchezaji huyu, ikizingatiwa kuwa ada ya uhamisho wake huenda ikawa ya kuvunja rekodi.