Mohamed Salah ahusishwa na dili la kujiunga na Besiktas, Darwin Nunez naye naye?
Hatua mpya katika mustakabali wa Mohamed Salah
Mustakabali wa nyota wa zamani wa Liverpool, Mohamed Salah, unaendelea kuteka vichwa vya habari huku taarifa mpya zikidai kuwa amefikia makubaliano ya awali na klabu ya Besiktas ya nchini Uturuki. Inaripotiwa kuwa klabu hiyo ya Istanbul inajiamini sana kuwa itafanikiwa kukamilisha usajili wake katika siku chache zijazo.
Ikumbukwe kuwa mwezi Machi, Liverpool ilithibitisha kuwa Salah ataondoka Anfield baada ya kukubaliana kusitisha mkataba wake mwaka mmoja kabla ya kumalizika rasmi, ili kumpa fursa ya kutafuta changamoto mpya nje ya England. Awali, ilidhaniwa kuwa mshambuliaji huyo angeelekea Saudi Arabia au Marekani (MLS), lakini upepo umeonekana kubadilika kuelekea Uturuki.
Mvutano wa taarifa na msimamo wa Besiktas
Taarifa za uhamisho huu zimekuwa na utata hivi karibuni. Wiki iliyopita, Besiktas ilitoa taarifa kali ikikanusha kuwepo kwa makubaliano yoyote na mchezaji huyo, huku ikimshutumu mwandishi wa habari aliyetoa taarifa hizo kwa kueneza habari za uongo.
Hata hivyo, mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, alifafanua kuwa hatua ya Besiktas kukataa taarifa hizo ilitokana na ukweli kwamba dili halikuwa limekamilika, si kwa sababu hawakuwa na nia. Romano alithibitisha kuwa Besiktas kweli imewasilisha ofa na iko kwenye mazungumzo, lakini ililazimika kuwa makini hadi makubaliano ya mwisho yapatikane.
Mkataba wa hadi 2027?
Kwa mujibu wa ripoti mpya kutoka kwa mwandishi wa habari wa Italia, Nicolo Schira, Besiktas sasa ina “makubaliano ya msingi” na Salah. Schira amedai kupitia mtandao wa X kuwa:
Mohamed Salah anazidi kuelekea Besiktas kama mchezaji huru. Kuna makubaliano ya msingi ya mkataba hadi mwaka 2027 (wenye mshahara wa Euro milioni 12 kwa mwaka) na chaguo la kuongeza hadi 2028. Kocha Italiano anashinikiza sana ili kumpata mchezaji huyo.
Darwin Nunez naye anaweza kuungana na Salah?
Si Salah pekee anayehusishwa na Besiktas. Ripoti nyingine inayoongeza msisimko ni ile ya mwandishi Sacha Tavolieri, aliyedai kuwa mshambuliaji mwingine wa zamani wa Liverpool, Darwin Nunez, naye yuko karibu kufikia makubaliano na klabu hiyo ya Uturuki kwa mkopo hadi mwisho wa msimu.
Iwapo taarifa hizi zitathibitika kuwa kweli, mashabiki wa Besiktas watakuwa na sababu ya kutabasamu kwa kupata huduma za nyota hawa wawili wa zamani wa The Reds. Sasa ni kusubiri hatua rasmi kutoka kwa pande zote husika katika siku hizi chache zijazo.