Morgan Rogers afunguka namna England itakavyomkabili Erling Haaland kwenye robo fainali
England uso kwa uso na Haaland
Safari ya England kuelekea nusu fainali ya Kombe la Dunia imepata changamoto kubwa: Erling Haaland. Nyota huyo wa Manchester City amekuwa mwiba mkali kwa mabeki wengi duniani, na England inajua vyema kuwa kuruhusu nafasi ndogo tu kwa mshambuliaji huyo inaweza kuwa mwisho wa ndoto yao.
Haaland, mwenye umri wa miaka 25, amekuwa na michuano bora hadi sasa akifunga mabao saba. Uwezo wake wa kutumia nguvu, kasi, na umakini mkubwa akiwa ndani ya eneo la hatari unawapa hofu wapinzani wake, akiwemo kiungo wa England, Morgan Rogers.
Mbinu ya kumzuia ‘nyota’ wa Norway
Alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu namna England itakavyomdhibiti mshambuliaji huyo hatari, Rogers alicheka kisha akajibu kwa uaminifu:
“Kuna mtu yeyote aliyewahi kumzuia Erling Haaland? Sijui kama yupo, lakini tutajaribu. Yeye ni mchezaji wa kipekee sana. Kwa takwimu anazoweka, unajua ni kwa kiasi gani alivyo bora. Tutalazimika kuzuia mipira inayomfikia ili asipate nafasi za kufunga, kwa sababu anakuwa hatari sana akiwa mbele ya lango.”
Rogers, ambaye anakipiga katika klabu ya Aston Villa, alikiri kuwa changamoto si kwa Haaland pekee, bali pia kwa wachezaji wengine wa Norway wanaocheza Ligi Kuu ya England, akiwemo nahodha wa Arsenal, Martin Odegaard.
England katika hali ya uchovu lakini morali juu
Baada ya ushindi wa kusisimua wa mabao 3-2 dhidi ya Mexico katika hatua ya 16 bora, kikosi cha England kimerudi katika kambi yao ya Kansas City kikiwa na uchovu mkubwa. Hata hivyo, Rogers anaamini kuwa wachezaji wamejipanga kuendelea kupambana.
“Ujumbe uliokuwepo katika mazoezi yetu ya kwanza ni kwamba tunapaswa kuendelea, tunataka zaidi, na tunaweza kuimarika zaidi. Kwa wengi wetu, hii itakuwa mechi kubwa zaidi kuwahi kushiriki, hususan katika hatua hii ya Kombe la Dunia,” aliongeza Rogers.
Umoja kikosini
Habari njema kwa ‘Three Lions’ ni kurejea kwa kiungo mkongwe Jordan Henderson baada ya kufanyiwa upasuaji wa mkono kufuatia jeraha alilolipata wakati wa kushangilia ushindi dhidi ya Mexico.
Rogers amemwezea Henderson kama “moyo” wa timu yao. “Kumuona akitabasamu asubuhi ya leo baada ya yote yaliyotokea ndani ya saa 48 zilizopita, ni jambo la kufurahisha sana kwetu. Yeye ndiye kiini cha umoja wetu,” alimalizia Rogers.
Wakati England ikijiandaa kwa mchezo huo wa Jumamosi mjini Miami, mashabiki wao wanaendelea kuhamasisha timu kwa wimbo wa ‘Wonderwall’ wa bendi ya Oasis, wimbo ambao Rogers anasisitiza kuwa kila Mwingereza anapaswa kuujua.