Sakata la Myles Lewis-Skelly lafikia tamati, kijana agoma kuondoka Arsenal
Sakata la Myles Lewis-Skelly lafikia tamati
Sakata la uhamisho lililochukua muda mfupi kumhusu nyota kijana wa Arsenal, Myles Lewis-Skelly, limefika tamati huku kukiwa na uhakika sasa wa wapi kijana huyu atakapocheza msimu ujao. Siku ya Jumanne, habari zilisambaa zikidai kuwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 19 amejitolea kubaki Emirates na kupambana kwa ajili ya nafasi katika kikosi cha Mikel Arteta.
Awali, kulikuwa na taarifa zilizodai kuwa mchezaji huyo amependekezwa kwa klabu za Manchester United na Chelsea, jambo lililoibua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki. Hata hivyo, imebainika kuwa kitendo hicho cha kuwekwa sokoni hakikutoka ndani ya klabu ya Arsenal, bali kiliaminika kufanywa na mawakala au watu wa kati waliokuwa wakimwakilisha mchezaji huyo.
Manchester United na Chelsea hawana nia
Taarifa kutoka The Times zimebainisha kuwa Manchester United walisogelewa kwa ajili ya kumsajili kijana huyo, lakini hawakuonyesha nia yoyote ya kufanya biashara hiyo. Imeelezwa kuwa awali katika dirisha la Januari, bei ya mchezaji huyo ilitajwa kufikia pauni milioni 60, kiasi ambacho United walikiona kuwa ni kikubwa mno.
Ingawa thamani yake sasa inatajwa kushuka hadi takriban pauni milioni 45, bado klabu hiyo ya Old Trafford haijaonyesha nia ya kumnasa, licha ya kuhitaji kuimarisha nafasi za beki wa kushoto na kiungo wa ulinzi ambazo ndizo Lewis-Skelly anazozicheza.
Kwa upande mwingine, The Athletic imeripoti kuwa hakuna uwezekano wa mchezaji huyo kutimkia Chelsea. Badala yake, Lewis-Skelly mwenyewe hana mpango wa kuondoka kwenye klabu yake ya utotoni.
Lewis-Skelly anataka kupambana
Kiungo huyo ambaye ni zao la akademia ya Arsenal, amedhamiria kubaki na kupigania namba katika kikosi cha kwanza chini ya Mikel Arteta. Licha ya ushindani mkali kikosini kutokana na ujio wa wachezaji wapya na uwepo wa nyota kama Declan Rice, Lewis-Skelly anaamini katika uwezo wake.
“Myles Lewis-Skelly anataka kubaki Arsenal na anazingatia kikamilifu kujiimarisha katika mipango ya kikosi cha kwanza cha Mikel Arteta kwa msimu ujao. Mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 19 anafurahia maisha Arsenal na hafikirii kuondoka,” ilieleza ripoti ya The Athletic.
Aidha, mchezaji huyo amekuwa akipata nafasi ya kuanza katika michezo ya maandalizi ya msimu (pre-season), jambo linaloonyesha kuwa bado ni sehemu ya mipango ya klabu hiyo. Kwa sasa, tetesi hizi zimezimwa rasmi, na mashabiki wa ‘The Gunners’ wanaweza kutarajia kumuona nyota huyo akiendelea kuwavaa jezi za klabu hiyo msimu ujao.