Nicky Butt amvaa Michael Carrick, adai anamuua Matheus Cunha
Mchambuzi Nicky Butt haoni matumaini kwa Carrick
Gwiji wa Manchester United, Nicky Butt, ametoa mtazamo mkali kuhusu mwenendo wa klabu hiyo chini ya kocha Michael Carrick. Katika kipindi cha The Good, The Bad and The Football, Butt alionyesha kutoridhishwa na jinsi Carrick anavyotumia kikosi chake, akilenga zaidi matumizi ya mshambuliaji Matheus Cunha.
Manchester United wameanza msimu huu kwa kusuasua, wakikusanya pointi tano pekee katika michezo mitano ya awali ya Ligi Kuu ya Uingereza. Hali hiyo imeleta shinikizo kwa Carrick ambaye alipewa mkataba wa kudumu baada ya kufanya vizuri kama kocha wa muda msimu uliopita.
‘Anamuua Cunha kwa kumpanga namba 9’
Hoja kuu ya Butt ni kwamba Matheus Cunha hawezi kucheza kama mshambuliaji wa kati (namba tisa) kwa ufanisi. Anaamini kuwa Carrick anapoteza ubora wa mchezaji huyo kwa kumlazimisha katika nafasi hiyo.
“Kumchezesha Cunha kama namba tisa kunamuua. Yeye si mchezaji yule unayemuona akicheza pembeni. Hatuna namba tisa mwingine zaidi ya Benjamin Sesko na Zirkzee, lakini Zirkzee naye hakuwa na uhakika kama anabaki au anaondoka, na hata anapoingia haonekani kama mshambuliaji anayeendana na viwango vya Manchester United,” alisema Butt.
Matatizo zaidi ya safu ya ulinzi
Sio Cunha pekee aliyepata lawama kutoka kwa mchezaji huyo wa zamani. Butt pia alionyesha wasiwasi mkubwa kuhusu safu ya ulinzi ya United, akidai kuwa viungo wa timu hiyo wanashindwa kutawala michezo na mabeki hawajafikia viwango vinavyohitajika kwa timu inayotaka kuwa mabingwa.
Aliongeza, “Safu ya ulinzi inaonekana ya kawaida tu. Beki wa kulia anatosha kutufikisha kwenye nafasi ya pili au ya tatu? Hapana. Harry (Maguire) ameshapita kilele chake. Martinez ni mchezaji mzuri lakini si beki wa kati anayeweza kutawala mchezo. Kuhusu Luke Shaw, tunajua anacheza mechi tatu au nne halafu anapata majeraha.”
Mvutano kuhusu majeraha ya Sesko
Katika mjadala huo, Butt na Paul Scholes walishangazwa na taarifa za majeraha ya Benjamin Sesko, ambayo yatamfanya akose kuitumikia timu yake ya taifa ya Slovenia.
Scholes alihoji kwa mshangao: “Inakuwaje mtu anapata majeraha ya mguu (shin)? Si huo ni mguu uliovunjika? Hivi huwezi kuvaa tu ‘shinpads’ ukaendelea kucheza?”
Butt aliongeza kuwa hali ya klabu kukosa mshambuliaji mwingine mbadala ni tatizo sugu linalohitaji ufumbuzi wa haraka ili timu iweze kupata matokeo mazuri kwenye michezo ijayo.