Nicky Butt amshauri Kobbie Mainoo kugomea mechi ya mshindi wa tatu ya England
Ujumbe mzito kwa Mainoo
Kiungo wa zamani wa Manchester United, Nicky Butt, ametoa ushauri mzito kwa kiungo kijana wa klabu hiyo, Kobbie Mainoo, akimwambia ajiondoe kwenye mchezo wa mshindi wa tatu wa Kombe la Dunia dhidi ya Ufaransa siku ya Jumamosi. Ushauri huu unakuja kufuatia Mainoo kukosa nafasi kabisa katika kikosi cha Thomas Tuchel tangu mashindano hayo kuanza.
Mainoo, ambaye alionyesha kiwango bora sana katika nusu ya pili ya msimu akiwa na United chini ya kocha Michael Carrick, amejikuta akiwa mtazamaji tu benchi katika mechi zote saba ambazo England imecheza kufikia hatua ya nusu fainali, ambapo walitolewa na Argentina.
”Mechi ya kijinga na haina maana”
Butt anaamini kuwa Tuchel amemtendea haki kidogo sana kijana huyo, na sasa anataka kumtumia kwenye mchezo usio na umuhimu mkubwa. Kwa mtazamo wa Butt, Mainoo haipaswi kujipotezea muda wala kuhatarisha afya yake kwa mechi hiyo.
“Sijui nini kinaendelea huko, kuna kitu hakiko sawa. Sasa wanataka kumchezesha kwenye mechi ya kijinga ya mshindi wa tatu. Mimi kama ningekuwa Kobbie Mainoo, ningegoma kucheza. Ningesema nimeumia. Hii ni mechi haina maana, hasa ukizingatia jinsi alivyotendewa,” alisema Butt.
Butt anaongeza kuwa ni hatari kwa Mainoo kuanza mechi hiyo baada ya kukaa nje kwa muda mrefu, jambo linaloweza kumsababishia majeraha yatakayomharibia msimu mzima wa ligi.
Tuchel yupo hatarini kufukuzwa
Mbali na suala la Mainoo, Nicky Butt amekuwa mkali sana kuhusu hatma ya Thomas Tuchel kufuatia kufeli kwa England kwenye Kombe la Dunia. Butt anaamini kuwa hakuna sababu ya kocha huyo Mjerumani kuendelea kuwepo kikosini.
“Huwezi kumweka hapo tena. Hakuna nafasi ya yeye kubaki baada ya kilichotokea. Anacheza soka la hovyo na la kujihami kupita kiasi, hata dhidi ya timu ambayo ilikuwa inafungika kama Argentina,” aliongeza Butt.
Kuhusu nani anayefaa kuchukua mikoba hiyo, Butt amependekeza majina ya Eddie Howe au Mauricio Pochettino. Anaamini kuwa Pochettino ana uwezo wa kurudisha heshima ya timu kutokana na uhusiano wake mzuri na mkurugenzi wa ufundi wa FA, John McDermott, pamoja na falsafa yake ya soka la kushambulia.