Oliver Glasner atua Nottingham Forest kama kocha mkuu
Mabadiliko makubwa City Ground
Nottingham Forest imekamilisha mchakato wa kumpata kocha mkuu mpya, Oliver Glasner, ambaye anakuwa kocha wa tano ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tu. Mwalimu huyo raia wa Austria mwenye umri wa miaka 51 anachukua mikoba ya Vitor Pereira, aliyeachishwa kazi siku ya Jumanne iliyopita.
Uteuzi huu ni sehemu ya mikakati ya klabu hiyo kujiimarisha kuelekea msimu wa 2026/27. Glasner, ambaye aliwahi kuinoa Crystal Palace, anatarajiwa kuleta utulivu katika benchi la ufundi ambalo limekuwa likibadilika mara kwa mara tangu msimu uliopita, likipitiwa na makocha kama Nuno Espirito Santo, Ange Postecoglou, na Sean Dyche.
Imani ya Glasner kwa Forest
Akizungumza baada ya kutambulishwa rasmi, Glasner alionyesha kufurahishwa na nafasi hiyo na kueleza imani yake kwa uongozi wa klabu hiyo.
“Nimefurahi sana kujiunga na Nottingham Forest kama kocha mkuu. Katika mazungumzo yangu ya kwanza na mmiliki pamoja na viongozi, ilikuwa dhahiri kuwa wana dira ya wazi kwa klabu hii na imani kubwa kwangu pamoja na benchi langu la ufundi ili tujenge mustakabali mzuri kwa muda mrefu.”
Aliongeza kuwa historia ya klabu hiyo, ikiwa ni pamoja na kushinda taji la Ulaya mara mbili, pamoja na hamasa ya mashabiki wake, ni vitu vilivyomshawishi kukubali changamoto hiyo.
Marinakis ammwagia sifa kocha mpya
Mmiliki wa klabu hiyo, Evangelos Marinakis, alibainisha sifa kuu tatu zilizomfanya amchague Glasner: uongozi wake, haiba yake, na mtindo wake wa kusakata soka.
“Oliver ni mshindi. Amepata mafanikio kupitia uongozi wake, haiba yake, na aina ya soka ambalo timu zake hucheza. Tunaamini yeye ndiye mtu sahihi wa kutuongoza katika sura hii mpya ya klabu.”
Marinakis alisisitiza kuwa lengo la klabu siyo tu kushindana katika Ligi Kuu ya England, bali ni kuirejesha Nottingham Forest katika nafasi ya juu miongoni mwa klabu zinazoheshimika barani Ulaya na England kwa ujumla. Kwa sasa, Glasner anatarajiwa kuanza kazi mara moja kwa kukutana na wachezaji na kuanza maandalizi ya msimu mpya (pre-season).