Pat Nevin aonya kuhusu kiwango cha Bradley Barcola ndani ya Liverpool
Kasi pekee haitoshi kwa Barcola?
Usajili wa Bradley Barcola kujiunga na Liverpool kutoka Paris Saint-Germain kwa kitita cha pauni milioni 123 ulikuwa moja ya habari kubwa katika dirisha la usajili lililopita. Hata hivyo, wakati mashabiki wengi wakimsubiri kwa hamu nyota huyo kuonyesha makali yake, mchambuzi wa soka na mchezaji wa zamani wa Chelsea, Pat Nevin, ametoa onyo kali kuhusu uwezo wa mchezaji huyo.
Nevin anaamini kuwa ingawa Barcola ni mchezaji mwenye kasi ya ajabu, bado ana safari ndefu ya kuwa mchezaji aliyekamilika kiufundi. Kwa mujibu wa Nevin, kasi hiyo ndiyo inayomfanya aonekane tishio, lakini inapokuja suala la ubunifu na maamuzi ya mwisho, kuna mapungufu dhahiri.
Mapungufu ya kiufundi yaliyomkuta Anfield
Tangu ajiunge na Liverpool, Barcola tayari ameanza kuonja joto ya jiwe katika Ligi Kuu ya England na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Nevin anaamini kuwa kuna sababu za msingi kwa nini mchezaji huyo hakuwa chaguo la kwanza kila mara akiwa PSG, na pia kwa nini anasubiri nafasi katika timu ya taifa ya Ufaransa.
“Nitajaribu kuelezea hili kwa upole: bado hajawa mchezaji aliyekamilika. Sio mbaya, lakini ana mapungufu madogo madogo kwenye mchezo wake. Inashangaza jinsi kasi yake inavyoweza kuficha mapungufu hayo,” alisema Nevin.
Nevin aliongeza kuwa ujuzi wa Barcola upo katika kiwango cha kawaida, lakini uwezo wake wa kusoma mchezo (vision) haujafika katika kiwango cha juu kinachotakiwa kwa klabu kubwa kama Liverpool.
Changamoto ya kukabiliana na timu zinazojilinda
Hoja nyingine nzito aliyoitoa Nevin ni namna Barcola atakavyoweza kuisaidia Liverpool dhidi ya timu zinazotumia ‘low block’ au kujilinda kwa wingi. Nevin anaonya kuwa kasi ya Barcola inafaa zaidi kwa timu zinazocheza mpira wa kushtukiza au zinazoshambulia kwenye nafasi zilizo wazi.
“Kama unacheza kwa ajili ya timu inayotafuta nafasi za kukimbia, ni vizuri sana. Lakini kama una kasi kubwa na unakutana na timu inayojilinda kwa ndani, hakuna nafasi ya kukimbia. Katika hali hiyo, unahitaji uwezo wa kiufundi na akili nyingi, sio kasi pekee,” aliongeza Nevin.
Kwa mashabiki wa Liverpool, hii ni angalizo la kutazama kwa umakini maendeleo ya mshambuliaji huyo huku akijaribu kuzoea presha kubwa ya soka la England. Muda pekee ndio utaonyesha kama Barcola ataweza kuongeza ubunifu zaidi kwenye mchezo wake ili kuendana na kasi yake ya ajabu.