Paul Merson amvaa Ollie Watkins kwa mgomo wake Aston Villa
Mgomo wa Watkins wazua gumzo
Staa wa zamani wa Arsenal na mchambuzi wa soka, Paul Merson, ametoa maneno mazito dhidi ya mshambuliaji wa Aston Villa, Ollie Watkins, kufuatia kitendo chake cha kukataa kucheza mchezo wa ufunguzi wa msimu dhidi ya Brighton. Katika mchezo huo ambao Villa walikubali kipigo cha mabao 4-0, timu hiyo ilikosa huduma ya mshambuliaji huyo huku kukiwa na taarifa kuwa alikuwa akishinikiza uhamisho wa kwenda klabu ya Al-Hilal ya nchini Saudi Arabia.
”Ni kitendo cha aibu”
Merson hakuficha hisia zake, akieleza kuwa kitendo hicho cha mchezaji kugoma kuingia uwanjani huku akiwa fiti ni jambo lisilokubalika katika soka la kulipwa. Alisisitiza kuwa wachezaji wanapaswa kuwaheshimu mashabiki wanaotumia fedha zao kuja uwanjani.
“Kama ni kweli kwamba Ollie Watkins alikuwa fiti kucheza dhidi ya Brighton lakini akakataa kujumuishwa, basi hilo ni jambo la aibu kubwa sana. Unalipwa kiasi kikubwa cha fedha, watu wamekaa Holte End wamelipia tiketi za msimu na kusafiri nchi nzima kukuunga mkono, alafu wewe huwezi kujitolea kucheza mechi moja?”
Merson aliongeza kuwa kazi ya soka ni ya bahati sana na mchezaji anapaswa kuthamini nafasi aliyonayo. “Una kazi bora kuliko zote duniani. Unacheza Premier League, unapata pesa nyingi, unalipwa ili uwe fiti. Nafahamu akili yake imehama kwa sababu ya ofa kubwa kutoka Saudi Arabia na umri wake umesonga, lakini ni lazima ufikirie pia mashabiki,” alisema Merson.
Makubaliano na Al-Hilal yafikiwa
Baada ya kuripotiwa kugoma kucheza, inaelezwa kuwa Watkins alirejea mazoezini Jumatatu na kuwaomba radhi wachezaji wenzake. Hata hivyo, inaonekana siku zake ndani ya Villa Park zimefika ukingoni.
Taarifa kutoka kwa mwandishi Sacha Tavolieri zinaeleza kuwa Aston Villa na Al-Hilal wamefikia makubaliano ya uhamisho wa staa huyo. Ingawa ada ya uhamisho haijawekwa wazi, inadaiwa kuwa Watkins atakuwa akijipatia mshahara wa takriban dola milioni 15 kwa mwaka nchini Saudi Arabia.
Aston Villa wajipanga na mrithi
Sababu kubwa iliyochelewesha dili hilo kukamilika mapema ilikuwa ni hitaji la Aston Villa kwanza kutafuta mshambuliaji wa kuziba pengo lake. Taarifa zinaashiria kuwa Nicolas Jackson ndiye chaguo la klabu hiyo kuchukua nafasi ya Watkins. Kwa sasa, mashabiki wa Villa wanasubiri kuona jinsi safu yao ya ushambuliaji itakavyokuwa baada ya kumpoteza mshambuliaji huyo aliyekuwa nguzo muhimu kwa misimu kadhaa.