Paul Parker amshauri Ten Hag kumuondoa Luke Shaw Man Utd
Shaw hafai tena Old Trafford?
Klabu ya Manchester United imetakiwa kufanya maamuzi magumu kuhusu nafasi ya beki wa kushoto, huku mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Paul Parker, akidai kuwa Luke Shaw hafai tena kuendelea kuchezea timu hiyo.
Shaw, ambaye amekuwa na majeraha ya mara kwa mara katika misimu ya hivi karibuni, anatajwa na Parker kama mchezaji ambaye amepoteza makali yake ya uwanjani. Ingawa beki huyo wa kimataifa wa Uingereza amekuwa na nyakati nzuri akiwa fiti, Parker anaamini kuwa kiwango chake kimeshuka kiasi cha kutoweza kuisaidia timu hiyo kwenye changamoto za sasa.
‘Hana kasi wala uwezo wa kukaba’
Akizungumza na Betarades.gr, Parker hakuficha hisia zake juu ya uwezo wa Shaw kwa sasa. Alieleza waziwazi kuwa United inahitaji beki mwenye kasi na uwezo wa kufanya kazi pande zote mbili za uwanja.
“Luke Shaw hawezi kukimbia, hawezi kukaba na hawezi kushambulia, sasa unamhitaji kwa kazi gani?” alisema Parker kwa masikitiko.
Parker aliongeza kuwa hata Diogo Dalot anapochezeshwa kama beki wa kushoto, bado kunakuwa na changamoto kubwa, hivyo ni dhahiri klabu inahitaji usajili wa dharura katika nafasi hiyo ili kuwa na uwiano mzuri.
Harry Amass ndiye mbadala?
Badala ya kutegemea soko la usajili pekee, Parker anapendekeza kuwa Manchester United inaweza kutumia vijana kutoka akademi yao, hususan Harry Amass. Parker anaamini kuwa ni wakati mwafaka kwa klabu hiyo kuwapa nafasi vijana wenye vipaji badala ya kung’ang’ania wachezaji wasiokuwa na viwango vya kuridhisha.
“Nimeona jinsi Harry Amass anavyocheza na mashabiki wamekuwa wakivutiwa sana na uwezo wake. Labda huu ndio wakati wa kumpa nafasi ya kucheza mfululizo. Klabu inapaswa kuwa bora katika kuwaibua na kuwatumia vijana kama yeye,” aliongeza Parker.
Kwa sasa, Manchester United inajiandaa kwa msimu mwingine mgumu, na maoni haya ya Parker yanakuja wakati ambapo klabu inatajwa kuwa sokoni kutafuta beki wa kushoto ili kuimarisha kikosi chao kabla ya msimu kushika kasi.