Paul Scholes ammwagia sifa James Maddison, amtaja kama chachu ya soka safi la Tottenham
Maddison ni muhimu kwa Tottenham
Kiungo mkongwe wa zamani wa Manchester United, Paul Scholes, ametoa mtazamo wake kuhusu mwenendo wa Tottenham Hotspur akisisitiza kuwa James Maddison ndiye mtu anayeweza kubadilisha taswira ya klabu hiyo uwanjani.
Katika mazungumzo yake kwenye podikasti ya The Good, The Bad and The Football, Scholes alionyesha kuvutiwa na uwezo wa Maddison wa kuchezesha timu. Kwa mujibu wa Scholes, kiungo huyo mwenye umri wa miaka 29 ana kipaji kikubwa kinachomfanya kuwa mhimili muhimu katika mifumo ya kocha Roberto De Zerbi.
“Mimi nampenda sana. Yeye ni mchezaji mzuri wa soka. Anafanya timu icheze soka safi, unajua ninachomaanisha? Lazima watafute namna ya kumtumia vyema uwanjani,” alisema Scholes.
Changamoto za Tottenham na mtazamo wa Nicky Butt
Wakati Scholes akimsifu Maddison, mwenzake Nicky Butt alizungumzia suala la usajili na mustakabali wa Spurs msimu huu. Butt alimtaja Sandro Tonali kama usajili bora zaidi uliofanywa na klabu hiyo katika dirisha lililopita la usajili.
Hata hivyo, Butt aliongeza kuwa kurejea kwa Maddison uwanjani baada ya kusumbuliwa na jeraha la goti (ACL) msimu uliopita, ni kama kupata mchezaji mpya ndani ya kikosi hicho.
“Kumbuka, Maddison amerudi baada ya kuwa majeruhi. Yeye ni kama usajili mpya. Atarejea na kuongeza nguvu. Wana wachezaji wa kiwango cha juu sana, kwa kweli wanao,” alisema Butt.
Je, Tottenham itatoka kwenye kipindi kigumu?
Scholes alibainisha kuwa Tottenham kwa sasa inapitia kipindi kigumu ambapo imekuwa na kawaida ya kupoteza michezo, tabia ambayo imeanza kuwa mzigo kwa timu hiyo kwa misimu miwili iliyopita. Licha ya changamoto hizo, anaamini kuwa muda utaongea.
“Wamekuwa na kawaida mbaya ya kupoteza michezo tangu msimu uliopita. Kwa sasa hawawezi kujinasua. Ni miaka miwili sasa. Hata hivyo, kuna wachezaji wazuri na nadhani kocha pia ni mzuri. Nadhani itachukua muda kidogo, pengine michezo sita, saba au nane ili mambo yakae sawa,” aliongeza Scholes.
Kwa sasa, mashabiki wa Spurs wanasubiri kwa hamu kumuona Maddison akirejea kikosini kikamilifu, hususan katika mchezo ujao dhidi ya Everton, huku kukiwa na matumaini kuwa ushindi wa mfululizo utaweza kuirejesha timu hiyo katika njia sahihi ya ushindani kwenye Ligi Kuu ya Uingereza.