Florentino Perez Afichua Mpango wa Real Madrid Kuvunja Rekodi ya Usajili kwa Euro Milioni 150 Kumleta 'Galactico' Mpya
Mchuano wa Urais Wapamba Moto Bernabeu
Uchaguzi wa urais wa Real Madrid unaotarajiwa kufanyika Jumapili hii umezidi kupamba moto, huku rais wa sasa, Florentino Perez, akitupa karata yake ya mwisho kwa kutangaza mpango mkubwa wa usajili. Perez amethibitisha kuwa klabu hiyo itatuma ofa ya kihistoria ya zaidi ya euro milioni 150 wiki ijayo kwa ajili ya kumsajili mchezaji mpya wa kiwango cha juu, maarufu kama ‘Galactico’.
Hatua hii ya Perez inakuja baada ya mpinzani wake mkuu katika uchaguzi huo, Enrique Riquelme, kufanya propaganda kubwa siku ya Jumatano usiku akiahidi kuwaleta mastaa wa Manchester City, Erling Haaland na Rodri, iwapo atashinda kiti hicho.
Riquelme na Ahadi ya Haaland Iliyobuma
Riquelme alionekana kwenye kipindi maarufu cha televisheni cha ‘El Hormiguero’ akionyesha jezi ya Real Madrid yenye jina la Erling Haaland mgongoni, huku akitoa ahadi nzito kwa wanachama takriban 95,000 wa Real Madrid wenye haki ya kupiga kura.
“Erling Haaland na Rodri watakuwa sajili zangu za kwanza za mastaa kama nitakuwa rais. Kama nikivunja ahadi yangu kuhusu wachezaji hawa wawili, nimesaini dhamana ambapo nitalipa asilimia 100 ya ada za uanachama kwa msimu ujao. Haaland ana kipengele cha kuondoka, na anataka kuja Madrid.”
Hata hivyo, ahadi hiyo ya Riquelme iligonga mwamba haraka sana. Baba mzazi wa Haaland pamoja na wakala wake walitoa taarifa ya pamoja kukanusha madai hayo, huku klabu ya Manchester City nayo ikiyafuta na kutishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mgombea huyo.
Perez Alipua Bomu Lake: Dumfries na Galactico wa €150m
Akizungumza siku ya Alhamisi kupitia kipindi cha ‘Horizonte’, Perez hakusita kumkejeli mpinzani wake huku akitangaza mikakati yake thabiti ambayo tayari imeanza kufanyiwa kazi. Kwanza, alithibitisha kuwa tayari wamewasilisha kiasi cha pauni milioni 20 ili kuamsha kipengele cha usajili cha beki wa kulia wa Inter Milan, Denzel Dumfries.
Hii inakuja baada ya kuthibitisha pia kuwa beki Ibrahima Konate atajiunga nao bure, na kocha wa zamani wa klabu hiyo, Jose Mourinho, atarejea kikosini.
“Mourinho na Konate wanakuja… na sasa nasema Dumfries. Ni beki wa kulia mzuri sana. Lakini tutakuwa na wachezaji wazuri pia kwenye nafasi nyingine,”
alisema Perez.
Kuhusu usajili wa ‘Galactico’ wa euro milioni 150, Perez alizua gumzo kubwa kwa kutoa mafumbo ya kusisimua kuhusu mchezaji huyo wa siri.
“Nitaenda kutoa ofa kwa klabu inayocheza Ligi ya Mabingwa hivi karibuni, siku ya Jumanne, ambayo itakuwa malipo makubwa zaidi kuwahi kufanywa na Real Madrid kwa ajili ya mchezaji katika historia yetu, angalau euro milioni 150.”
“Sio [Jeremy] Doku na wala sio [Erling] Haaland, sio [Harry] Kane, wala sio [Michael] Olise… Ofa hiyo ya euro milioni 150 sio kwa ajili ya mlinzi. Anaweza kuwa kiungo au mshambuliaji. Ni mchezaji mdogo (kijana). Na hachezi Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League). Ni ‘Galactico’ wa kweli.”
Perez alisisitiza kuwa wao wanafanya kazi kwa weledi tofauti na mpinzani wake:
“Lakini kwanza tutazungumza na klabu yake, hatutafanya yale aliyofanya yule bwana (Riquelme). Kuhusu dili la Haaland? Kila mtu anayehusika alikanusha. Wakala wake, baba yake, klabu yake, kila mtu. Yalikuwa ni maneno ya uongo tu.”
Kurejea kwa Jose Mourinho ‘The Special One’
Kando na usajili wa wachezaji, kurejea kwa Jose Mourinho kwenye benchi la ufundi la Real Madrid kumeleta msisimko mkubwa miongoni mwa mashabiki. Mourinho, ambaye aliondoka klabuni hapo miaka kadhaa iliyopita, anatajwa na Perez kama mtu sahihi wa kurejesha utamaduni wa ushindi na ushindani mkali kikosini.
“Nimefurahi sana, Mourinho ndiye mtu aliyetufanya tuwe washindani tena, alijenga ule moyo wa kupambana uliotufanya tushinde mataji sita ya Ligi ya Mabingwa baada yake kuondoka. Sasa tunataka arejeshe moyo huo huo wa ushindani hapa,”
alieleza Perez.
Mchuano huu wa kiti cha urais wa Real Madrid umekuwa moja ya matukio yanayofuatiliwa zaidi ulimwenguni, ukionyesha jinsi siasa za klabu hiyo kubwa zinavyoweza kutikisa soko la usajili la soka duniani. Mashabiki wa soka nchini Tanzania na kote duniani sasa wanasubiri kwa hamu kuona kama Perez atashinda uchaguzi huo wa Jumapili na kutekeleza ahadi yake ya kumtambulisha mchezaji huyo wa siri siku ya Jumanne.