Emmanuel Petit: Victor Osimhen ataleta kitu tofauti Arsenal kuliko Alvarez
Petit aona tofauti kati ya Osimhen na Alvarez
Kiungo wa zamani wa Arsenal, Emmanuel Petit, ametoa mtazamo wake kuhusiana na tetesi za klabu hiyo kutafuta mshambuliaji mpya kabla ya dirisha la usajili kufungwa. Wakati Julian Alvarez akionekana kutotua Emirates, jina la Victor Osimhen limeibuka kama mbadala sahihi wa kuimarisha safu ya ushambuliaji ya Mikel Arteta.
Petit, ambaye aliwahi kuchezea The Gunners, anaamini kuwa wachezaji hawa wawili wana uwezo tofauti ambao wanaweza kuipa timu mbinu mbadala kulingana na mahitaji ya mchezo.
Akizungumzia ubora wa Alvarez, Petit alisema:
“Yeye ni mchezaji mzuri mwenye harakati nzuri uwanjani na akili nyingi. Ana kasi, ufundi, na maono. Anaweza kufunga magoli mengi na kutoa pasi za magoli. Ni vigumu wakati mwingine kupata wachezaji wenye akili wanaoelewa DNA ya timu. Arsenal wana DNA halisi uwanjani, na nadhani Alvarez angekuwa sahihi kwa Arsenal.”
Nguvu ya Osimhen ni hitaji jingine
Kwa upande mwingine, Petit anaona kuwa Victor Osimhen, ambaye kwa sasa anakipiga Galatasaray, ataleta kitu ambacho Arsenal huenda inakikosa kwa sasa.
“Osimhen ni mchezaji tofauti, hana sifa zilezile kama Alvarez. Yeye ataleta nguvu ya ziada katika safu ya ushambuliaji. Ni mchezaji mwenye kasi, mpiganaji, na mwenye utu wa kipekee. Analeta kitu tofauti kabisa na Alvarez. Mlete! Wao ni chaguo mbili tofauti, lakini nawakubali wote wawili.”
Alvarez kwa sasa anaonekana kubaki Atletico Madrid, huku uvumi ukionyesha kuwa Barcelona walikuwa kipaumbele chake, hali inayofanya ndoto za Arsenal kumsajili nyota huyo kutoka Argentina kuwa ngumu kutimia.
Ushauri kuhusu Myles Lewis-Skelly
Sio suala la washambuliaji tu, Petit pia amegusia hatima ya chipukizi Myles Lewis-Skelly ambaye amekuwa akihusishwa na kuondoka. Licha ya ripoti zilizokuwa zikidai mchezaji huyo angeweza kuelekea Chelsea au Manchester United, Petit anaamini kinda huyo anapaswa kubaki.
“Itakuwa ni kupoteza kipaji kama ataondoka, ingawa siwezi kusema ni pengo kubwa sana kwa sasa kwa sababu kikosi kina wachezaji wengi wenye vipaji wanaoweza kucheza nafasi tofauti,” alisema Petit.
Ameongeza kuwa uwezo wa Lewis-Skelly kucheza nafasi nyingi, ikiwemo kiungo na beki wa kushoto, ni faida kwa Arteta. Licha ya ushindani mkali wa namba katika kikosi cha Arsenal, Petit anasisitiza kuwa ni vyema klabu imtunze kinda huyo ili aendeleze kipaji chake Emirates.