Mauricio Pochettino afunguka uwezekano wa kuifundisha England na kurejea Tottenham
Pochettino na ndoto ya kuinoa England
Kocha wa timu ya taifa ya Marekani, Mauricio Pochettino, ameweka wazi kuwa yupo tayari kuinoa timu ya taifa ya England siku za usoni kama mambo yatakuwa sawa na yeye akiwa hana timu nyingine ya kufundisha.
Pochettino, ambaye kwa sasa ana mkataba na Marekani hadi kumalizika kwa Kombe la Dunia la mwaka 2030, amesema kuwa uzoefu wake mkubwa unamfanya ajione anaweza kufanya kazi hiyo. Hata hivyo, alisisitiza kuwa hayupo tayari kwa sasa kwani ana majukumu yake ya kuitumikia Marekani.
Akizungumza na ESPN, kocha huyo raia wa Argentina aligusia pia utata wa yeye kuwa Mwaargentina na kuwahi kuwepo kwa historia ngumu kati ya nchi yake na England, lakini akaamini kuwa soka linapita mipaka hiyo.
“Kwa sasa kutokana na uzoefu wetu, labda ndiyo. Kama nitakuwa huru huko mbeleni, kwa nini isiwezekane? Soka lina shauku inayofanana kila mahali. Mimi ni Mwaargentina, lakini nimefanya kazi England na niliipenda, hivyo kwangu sioni kama kuna tatizo katika kutetea bendera ya nchi nyingine kupitia soka,” alisema Pochettino.
Mapenzi ya dhati kwa Tottenham
Sambamba na hilo, Pochettino alizungumzia uhusiano wake wa kipekee na klabu ya Tottenham Hotspur aliyoiongoza kati ya mwaka 2014 na 2019. Kocha huyo amekiri kuwa Tottenham ni klabu pekee ambayo yupo tayari kuisaidia katika hali yoyote, hata kama wangekuwa wanacheza ligi ya daraja la chini.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kurejea klabuni hapo, Pochettino alibainisha kuwa changamoto kubwa mara nyingi imekuwa ni muda (timing). Wakati alipokuwa huru, hakuwahi kupata mawasiliano kutoka Tottenham, na wakati alipokuwa na kazi, ndipo ofa zilipokuwa zinakuja.
“Tatizo lilikuwa ni muda. Wakati niko huru, sikuwa napata mawasiliano, na nilipokuwa nafanya kazi, ndipo mawasiliano yanakuja. Labda siku moja nyota zitakaa sawa na hilo litawezekana. Kama nitakuwa huru, bila shaka nitarudi. Tottenham ni klabu ambayo nipo tayari kuisaidia wakati wote, hata wakiwa daraja la chini,” aliongeza kocha huyo.
Pochettino kwa sasa anaendelea na jukumu lake la kuijenga timu ya taifa ya Marekani, akilenga kuifikisha timu hiyo kwenye mafanikio makubwa katika michuano ijayo ya Kombe la Dunia, huku Thomas Tuchel akiendelea na jukumu lake la kuiongoza England hadi kumalizika kwa michuano ya Euro 2028.