Real Madrid yafanya mawasiliano na Man Utd kwa ajili ya kinda JJ Gabriel
Real Madrid yatafuta saini ya kinda hatari wa Man Utd
Klabu ya Real Madrid imeripotiwa kuanza mawasiliano rasmi na Manchester United kuhusu uwezekano wa kumsajili kinda hatari, JJ Gabriel. Kijana huyo mwenye umri wa miaka 15 amekuwa gumzo kubwa baada ya kutoa ombi rasmi kwa United kutaka mkataba wake usitishwe ili aweze kuwa mchezaji huru.
Hata hivyo, Manchester United wameonekana kugoma kukubali ombi hilo la kinda huyo. Gabriel, ambaye anatajwa kuwa mmoja wa wachezaji bora kuwahi kutokea katika akademi ya United katika miaka ya hivi karibuni, anatarajiwa kufikisha umri wa miaka 16 mwezi ujao, hatua ambayo inaweza kurahisisha kuondoka kwake.
Kipaji cha kipekee kinachovutia vigogo
Gabriel amekuwa na kiwango bora ndani ya timu ya vijana ya United (U-18), ambapo amefanikiwa kufunga mabao 29 katika michezo 32. Uwezo wake wa kucheza kama mshambuliaji, winga, na kiungo mshambuliaji umemvutia Ryan Giggs, aliyemuelezea kijana huyo kama “kipaji cha kipekee cha kizazi hiki.”
Kocha mmoja wa vijana aliyewahi kufanya naye kazi alisema:
“Ana uwezo mkubwa wa kuzunguka na mpira, ni mfungaji mzuri na anatumia miguu yote miwili. Anapenda kufunga mabao na muda wote anataka kujifunza. Ni mtoto mwenye nidhamu na tabasamu kila wakati.”
Hatari ya kwenda Real Madrid
Licha ya kuvutiwa na vilabu vikubwa kama Real Madrid na Barcelona, wapo wanaohoji kama ni uamuzi sahihi kwa kijana huyo kuondoka England akiwa bado mdogo. Gwiji wa Liverpool, Steven Gerrard, ametoa angalizo kupitia TNT Sports.
Gerrard alisema:
“Tuchukulie mfano wa Jose Mourinho huko Real Madrid. Hata kama JJ Gabriel akielekea huko, je, Mourinho atampa nafasi ya kucheza moja kwa moja? Makocha wa kiwango cha juu wanawatumia vijana pale wanapokuwa tayari kuchangia timu. Nahisi kuna haraka isiyo ya lazima hapa.”
Kwa sasa, vyombo vya habari nchini Hispania vinaripoti kuwa Real Madrid wako makini kufuatilia hatua za kijana huyo, wakijua kuwa kutokuwepo kwa mkataba wa kitaalamu na United kunaweza kuifanya dili hiyo iwe rahisi zaidi. Dunia ya soka inasubiri kuona hatma ya kinda huyu ambaye amekuwa gumzo kubwa barani Ulaya.