Ronaldo: Hispania wataibuka kidedea kwa urahisi dhidi ya Argentina kwenye fainali ya Kombe la Dunia
Utabiri wa Ronaldo kuhusu fainali ya Kombe la Dunia
Legend wa soka wa Brazil, Ronaldo Nazario, ameweka wazi mtazamo wake kuelekea mchezo mkubwa wa fainali ya Kombe la Dunia unaotarajiwa kupigwa New Jersey kati ya Hispania na Argentina. Kwa mujibu wa mshambuliaji huyo wa zamani, Hispania ina kila sababu ya kutwaa ubingwa huo kwa namna wanavyocheza soka lao kwa sasa.
Hispania imekuwa kwenye kiwango cha juu sana kuelekea fainali hii, hasa baada ya kuiondosha Ufaransa kwa mabao 2-0 kwenye nusu fainali. Kwa upande mwingine, Argentina ililazimika kupambana kwa nguvu na kurudisha bao ili kuifunga England na kufika hatua hii.
Ubora wa Hispania na falsafa ya Guardiola
Ronaldo, ambaye alikuwa akizungumza na mchezaji mwenzake wa zamani wa Brazil, Denilson, anaamini kuwa Hispania haitapata shida yoyote mbele ya Argentina. Alisema waziwazi:
“Nafikiri Hispania itashinda na mchezo utakuwa rahisi. Kwangu mimi, Ufaransa na Hispania ndizo zilikuwa timu bora tangu mwanzo. Hispania wanacheza soka la kipekee na DNA yao inafahamika vyema; wamekua wakicheza hivi kwa muda mrefu sana.”
Ronaldo aliongeza kuwa mafanikio ya sasa ya Hispania yanaakisi falsafa iliyoanzishwa na Pep Guardiola miaka ya nyuma akiwa Barcelona. Kwake, mfumo wao wa kuuchezea mpira kwa kasi, kutulia na kuudhibiti mchezo ndio silaha kubwa itakayowapa ushindi.
Argentina bado ni hatari lakini…
Ingawa Ronaldo anaikubali Argentina na juhudi za Lionel Messi, ambaye amefunga mabao nane katika michuano hii, haoni kama watakuwa na uwezo wa kuizuia Hispania. Ronaldo anaamini kuwa uwezo wa Argentina wa kupindua matokeo dhidi ya timu kama Misri na England hautoshi kuwapa ubingwa mbele ya kikosi cha Hispania.
“Siamini kama Argentina ina nguvu ya kuhimili mchezo huu, kwa sababu Hispania itakuwa na mpira miguuni mwao muda mwingi. Njia wanayocheza Hispania imekaa kiotomatiki; hakuna haraka, wanacheza kwa kasi, wanatawala mchezo na wanajua jinsi ya kupooza presha kwa kumiliki mpira,” aliongeza Ronaldo.
Ingawa Ronaldo anasifu roho ya ushindi na tabia ya kutokukata tamaa ya Argentina inayoongozwa na Messi, anasisitiza kuwa ubora wa kiufundi wa Hispania utakuwa na maamuzi makubwa katika mchezo huo wa fainali.