Roy Keane amlipukia Phil Foden kwa kuwachokoza mashabiki wa Man Utd
Hasira za Roy Keane baada ya sakata la Old Trafford
Hadithi ya kadi nyekundu aliyoipata Phil Foden katika mchezo wa watani wa jadi wa Manchester (Manchester Derby) imeendelea kuchukua sura mpya. Safari hii, si kuhusu maamuzi ya mwamuzi Michael Oliver, bali ni tabia ya mchezaji huyo nje ya uwanja ambayo imemkera gwiji wa Manchester United, Roy Keane.
Foden alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Bruno Fernandes. Ingawa Keane awali alionekana kumtetea Foden akidai kuwa kadi hiyo haikustahili na kwamba Fernandes ndiye aliyekuwa na mchezo wa kihuni, msimamo wake umebadilika ghafla baada ya kuona video iliyosambaa mitandaoni.
Uchokozi katika eneo la maegesho
Katika video hiyo iliyosambaa, Foden alionekana akipita kuelekea kwenye basi la timu yake huku akiwaonyesha ishara ya ‘1-0’ kwa vidole mashabiki wa Manchester United waliokuwa nje ya uwanja wa Old Trafford. Kitendo hiki kimeonekana kumuudhi sana Keane ambaye anaona mchezaji huyo alipaswa kujiheshimu zaidi.
Akizungumza kwenye kipindi cha The Overlap, Keane alisema:
“Naweza kutoa hoja kuhusu Foden? Foden anapata kadi nyekundu mwishoni mwa juma na anaachwa nje ya kikosi cha timu ya taifa ya England. Halafu unamuona akipita kuelekea kwenye basi, anainua vidole kuonyesha 1-0 kwa mashabiki wa United. Unafanya nini? Ingia kwenye basi.”
Mgongano wa mitazamo
Katika mjadala huo, Jill Scott alijaribu kumtetea Foden kwa kusema kuwa ni kawaida kwa mchezaji kujibu mapigo pale anaposhambuliwa kwa maneno na mashabiki, akisisitiza kuwa Foden ni shabiki damu wa Manchester City tangu utotoni.
Hata hivyo, Keane hakuwa tayari kusikiliza utetezi huo, akisisitiza kuwa mchezaji anapokuwa amepata kadi nyekundu na timu yake inapata ushindi wa utata, anapaswa kuwa na busara na kuepuka mambo yanayoweza kuongeza joto na migogoro isiyo ya lazima. Kwa Keane, kitendo cha Foden kilikuwa cha utoto na hakikustahili kufanywa na mchezaji anayechezea ngazi ya juu kabisa ya soka.