Ryan Giggs amtaja staa anayemvutia zaidi ndani ya Arsenal
Odegaard anawavutia wengi
Gwiji wa klabu ya Manchester United, Ryan Giggs, ameweka kando upinzani wa jadi na kuelezea kuvutiwa kwake na kiungo mshambuliaji wa Arsenal, Martin Odegaard. Kwa mujibu wa Giggs, nyota huyo wa Norway ndiye mchezaji anayemvutia zaidi katika kikosi cha sasa cha Mikel Arteta.
Odegaard, ambaye alikuwa na changamoto za majeraha msimu uliopita, amerejea kwenye ubora wake na kuonyesha uwezo mkubwa uwanjani. Mpaka sasa, ameshafunga mabao manne katika michezo sita aliyocheza katika mashindano yote, ikiwemo ile ya Ngao ya Jamii.
Upekee wa Odegaard uwanjani
Akizungumza kwenye chaneli ya YouTube ya Rio Ferdinand, Giggs hakusita kumsifu nahodha huyo wa Arsenal kwa jinsi anavyochezesha timu.
“Odegaard ndiye mchezaji anayenivutia zaidi kwa sasa. Anaonekana kama anayeimiliki michezo yote. Anashuka chini kuchukua mipira kutoka kwa mabeki, anafanya kukimbia kuelekea mbele, na yupo kila mahali uwanjani.”
Giggs aliongeza kuwa mbali na ubunifu, Odegaard ana mchango mkubwa hata kwenye safu ya ulinzi.
“Ni mzuri sana kuzuia, ananyang’anya mipira na anapambana sana. Anaonekana mwenye nguvu na utulivu mkubwa anapokuwa na mpira miguuni mwake.”
Imani kwa Kai Havertz
Wakati Giggs akimvulia kofia Odegaard, nyota mwingine wa Arsenal, Kai Havertz, naye amepata sifa kutoka kwa mchambuzi wa soka na winga wa zamani wa Chelsea, Pat Nevin. Nevin anaamini kuwa Havertz ana uwezo wa kuwa miongoni mwa wafungaji bora wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.
Nevin anaamini kuwa kupata maandalizi mazuri ya msimu (pre-season) kumeleta mabadiliko makubwa kwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Chelsea.
“Nampenda sana Kai Havertz kama mchezaji. Ni mchezaji mahiri sana. Sasa hivi anaonekana ametulia, amepata nafasi ya kufanya mazoezi ya kutosha kabla ya msimu na ana timu nzuri sana nyuma yake inayomsaidia.”
Nevin aliongeza kuwa ingawa ni hatua kubwa, hatashangaa kuona Havertz akimaliza msimu akiwa mfungaji wa pili bora wa ligi hiyo. “Sifikiri kama jambo hilo haliwezekani, ninaamini ana uwezo wa kufanya hivyo,” alisisitiza Nevin.