Sandro Tonali Aitolea Nje Spurs, Atamani Kujiunga na Arsenal ya Mikel Arteta
Mbio za kuwania saini ya kiungo wa kimataifa wa Italia na klabu ya Newcastle United, Sandro Tonali, zimechukua sura mpya. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 anaripotiwa kupendelea zaidi kujiunga na Arsenal kuliko mahasimu wao wa London Kaskazini, Tottenham Hotspur, iwapo ataondoka St. James’ Park msimu huu wa joto.
Baada ya msimu mgumu na wa kusikitisha wa 2025/26 kwa Newcastle United, mustakabali wa Tonali klabuni hapo unaonekana kufikia ukingoni. Klabu za Arsenal, Tottenham Hotspur, na mabingwa watetezi Manchester City zote zinapigana vikumbo kuwania huduma ya kiungo huyo mbunifu.
Tonali Kuvutiwa na Mradi wa Mikel Arteta
Ingawa Tottenham ndiyo klabu inayoonyesha nia kubwa zaidi na iko tayari kufanya kazi na kocha wao raia wa Italia, Roberto De Zerbi, ripoti mpya zinadai kuwa Tonali anaiangalia zaidi Arsenal.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka gazeti la The Daily Mail, iwapo Arsenal wataamua kuonyesha nia thabiti na kuwasilisha ofa rasmi, Tonali atachagua kwenda Emirates Stadium kufanya kazi chini ya Mikel Arteta badala ya kutua Tottenham.
Meneja wa Arsenal, Mikel Arteta, pamoja na Mkurugenzi wa Michezo, Andrea Berta, wanapanga kuimarisha safu yao ya kiungo, na jina la Tonali limekuwa miongoni mwa majina yanayofuatiliwa kwa karibu sana.
Dau la Pauni Milioni 75 la Spurs Yakataliwa
Mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, amefichua kuwa Tottenham tayari wameshawasilisha ofa rasmi ya pauni milioni 75 kwa ajili ya Tonali, lakini ofa hiyo ilikataliwa mara moja na uongozi wa Newcastle United.
Mwandishi wa habari Ben Jacobs naye ameongeza kuwa Spurs hawajakata tamaa na wanapanga kurudi tena na ofa iliyoboreshwa, huku Manchester City nao wakiendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya mchezaji huyo ili kufanya maamuzi yao.
Shearer na Agbonlahor Washangazwa na Tetesi za Spurs
Uamuzi wowote wa Tonali kujiunga na Tottenham utawashangaza wengi, hasa kutokana na kiwango cha klabu hiyo katika misimu ya hivi karibuni. Nguli wa Newcastle United, Alan Shearer, ameeleza kuwa uhamisho wa kwenda Spurs hautakuwa na tija kwa kiungo huyo mahiri.
Shearer alisema:
“Tottenham wameepuka kushuka daraja hivi punde. Naelewa mvuto wa jiji la London, lakini kwenda Spurs ambao wamemaliza chini sana kwenye msimamo kwa miaka miwili iliyopita, itakuwa hatua ya kushangaza katika taaluma ya Tonali kwa mtazamo wangu. Lakini sishangai kama ni kweli ametoa ishara ya kutaka kuondoka Newcastle. Kama hataki kubaki, unaweka bei unayotaka na kama kuna mtu yuko tayari kulipa—ambayo inaonekana itabidi iwe tarakimu tatu—basi unasema asante sana, unachukua pauni milioni 100 na ushee kisha maisha yanaendelea.”
Mchezaji wa zamani wa Aston Villa na mchambuzi wa soka, Gabriel Agbonlahor, naye alikosoa vikali uwezekano wa Tonali kujiunga na Spurs akishindwa kuelewa mantiki ya mchezaji huyo kuondoka Newcastle kwenda timu inayofanya vibaya.
Agbonlahor akizungumza kupitia TalkSPORT alisema:
“Kwa nini Tonali atake kwenda kwenye timu inayoshika nafasi ya 17? Spurs sio timu ya sita bora tena. Wamehitimisha misimu miwili mfululizo wakiwa nafasi ya 17 kwenye ligi. Sielewi kabisa, na nadhani anamwambia wakala wake, ‘Samahani, nani anayevutiwa na mimi? Nilidhani naenda kwenye klabu kubwa ya Ulaya inayocheza Ligi ya Mabingwa. Nifanyie wepesi, siwezi kwenda Spurs.’”
Vita hii ya usajili inatarajiwa kupamba moto zaidi katika wiki zijazo, huku Arsenal wakiwa kwenye nafasi nzuri ya kumshawishi Tonali iwapo tu watafikia makubaliano ya ada ya usajili na Newcastle United.