Solskjaer amuunga mkono Carrick, afichua alijitolea kurejea Man Utd
Solskjaer bado ana imani na Carrick
Ole Gunnar Solskjaer amesema anaamini Michael Carrick ana uwezo wa kuiongoza Manchester United na kuisogeza klabu mbele, licha ya mwanzo mgumu wa kocha huyo katika msimu huu.
Solskjaer, aliyewahi kuinoa United na pia kufanya kazi na Carrick akiwa msaidizi wake, amemtaja kuwa mtu anayefaa kwa kazi hiyo. Kwa mujibu wa kocha huyo wa zamani, Carrick anauelewa wa kutosha kuhusu klabu, mashabiki wake na matarajio yanayoambatana na kuiongoza timu hiyo.
Akizungumza na chombo cha habari cha Norway, TV2, Solskjaer alieleza kuwa Carrick ana ukali na ari ya ushindani ambayo huenda isionekane kwa urahisi kwa watu wa nje.
“Michael ana kila kinachohitajika kuisogeza klabu hiyo mbele. Nafikiri ndiye mtu sahihi.”
Aliongeza kuwa Carrick anaielewa klabu na mashabiki wake, huku akijua pia kinachohitajika ili kufanikiwa. Solskjaer alisema wawili hao wanafanana kwa namna nyingi, na kwamba wote wana ile “shetani” ya ndani inayohitajika kupambana na changamoto za kazi hiyo.
Carrick anakabiliwa na presha ya matokeo
Man Utd ilimchagua Carrick badala ya Solskjaer kuwa kocha wa muda baada ya Ruben Amorim kuondoka mwanzoni mwa mwaka. Baadaye, Carrick alipewa nafasi ya kuwa kocha wa kudumu baada ya kuisaidia timu kumaliza nafasi ya tatu kwenye Premier League na kufuzu Ligi ya Mabingwa.
Hata hivyo, mwanzo wa msimu huu haujawa mzuri. United imeshinda michezo miwili pekee kati ya 13 iliyocheza, hali iliyoongeza presha kwa Carrick na kuibua maswali kuhusu mustakabali wake.
Timu hiyo inatarajiwa kukutana na AS Roma na Aston Villa nyumbani kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa. Matokeo mabaya katika michezo hiyo yanaweza kuongeza zaidi shinikizo kwa kocha huyo, ambaye aliwahi kuwa msaidizi wa Solskjaer katika klabu hiyo.
Pamoja na changamoto hizo, Solskjaer amesisitiza kuwa bado anaamini Carrick anaweza kufanikiwa. Alisema wakati yeye mwenyewe alipokuwa akizungumza na viongozi wa United, alimwelezea Carrick kama mtu mzuri na mwenye sifa za kuiongoza timu.
Solskjaer afichua mazungumzo na viongozi wa United
Solskjaer pia ameeleza kuwa alizungumza na Jason Wilcox na Omar Berrada wakati Man Utd ilipokuwa ikitafuta kocha baada ya kuondoka kwa Amorim. Alisema mazungumzo hayo hayakufika kwenye majadiliano ya mkataba wala muda wa kuinoa timu.
“Nilijitolea kuingilia kati kama ingehitajika, na sikuweka masharti yoyote. Nilieleza mawazo yangu kuhusu kile kinachohitajika ili klabu isonge mbele. Tulikuwa na mazungumzo mafupi; hakukuwa na mazungumzo ya mkataba.”
Solskjaer alisema hakutaka kazi hiyo kwa udi na uvumba, lakini angekubali kusaidia kama klabu ingemwomba. Alisema hali hiyo ilikuwa sawa pia kwa Carrick, ambaye aliamini angekuwa tayari kukubali jukumu hilo.
Kocha huyo wa zamani alifutwa kazi na United baada ya kuiongoza kwa kipindi alichokieleza kuwa maalumu, chenye nyakati nzuri. Alikiri kuwa bado anaikumbuka klabu na angeweza kujiona akiendelea kubaki Old Trafford kwa muda mrefu, lakini anaamini kila kipindi huwa na mwisho wake.
Alisema angerudi kuisaidia timu kwa muda kama angepewa nafasi mwezi Januari, lakini hakutarajia kuendelea na kazi hiyo zaidi ya majira ya kiangazi. Solskjaer pia alikiri kuwa ana hisia za kuwa na mambo ambayo hayajakamilika akiwa United, na kwamba angefurahia kupata nafasi nyingine ya kuinoa klabu hiyo siku moja.