Steven Gerrard ampa onyo zito kinda wa Man Utd, JJ Gabriel
Shinikizo la kutaka kuondoka Man Utd lamtia hofu Gerrard
Hali ya sintofahamu imetanda ndani ya klabu ya Manchester United baada ya kinda wao mwenye kipaji kikubwa, JJ Gabriel, kuripotiwa kuomba kuondoka klabuni hapo. Kinda huyu mwenye umri wa miaka 15, ambaye anatarajiwa kutimiza miaka 16 mwezi ujao, anatajwa kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea katika akademi ya klabu hiyo.
Taarifa zinaeleza kuwa Gabriel, ambaye aling’ara kwa kufunga ‘hat-trick’ kwenye mchezo wake wa kwanza wa UEFA Youth League dhidi ya FC Sabah, amewasilisha ombi rasmi la kutaka kuvunja mkataba wake ili kuwa mchezaji huru. Hatua hii imewashangaza wengi kwani kinda huyo amekuwa na klabu hiyo tangu akiwa na umri wa miaka 11.
Gerrard atoa angalizo
Gwiji wa Liverpool, Steven Gerrard, ameibuka na kuonyesha kusikitishwa na hatua ya kinda huyo na wale wanaomzunguka kukurupuka. Akizungumza na TNT Sports, Gerrard anaamini kuwa Man Utd ndipo mahali sahihi kwa Gabriel kukuza kipaji chake.
“Sio tu katika hali hii, lakini kwa ujumla inanishitua kuona jinsi wachezaji chipukizi wanavyokimbizwa na kulazimishwa katika hatua za haraka za soka. Sijui undani wa suala hili la JJ Gabriel, lakini kiukweli yuko kwenye moja ya klabu kubwa duniani yenye utamaduni wa kuzalisha wachezaji mahiri,” alisema Gerrard.
Ulinzi na subira kwa chipukizi
Gerrard aliongeza kuwa uwepo wa makocha kama Michael Carrick na Steve Holland ni faida kubwa kwa kinda huyo, kwani wana uwezo wa kumkinga na kumpa nafasi pale tu atakapokuwa tayari.
“Kuna watu makini nyuma ya pazia pale Manchester United. Kama huyu mtoto angekuwa tayari, angetumika. Lakini kwa nje, suala hili linaonekana kama kuna shinikizo kutoka kwa watu wanaomzunguka kama mawakala au wazazi, jambo ambalo linaweza kuharibu maendeleo ya kinda huyu,” aliongeza Gerrard.
Hofu ya ‘mzigo’ kwa klabu nyingine
Mbali na maslahi ya mchezaji, Gerrard alionya kuwa shinikizo hili linaweza kuleta ‘mzigo’ kwa klabu yoyote itakayojaribu kumsajili, kwani makocha wakubwa hawapendi kulazimishwa kuchezesha wachezaji ambao bado hawajakomaa kiushindani.
Kwa sasa, ulimwengu wa soka unasubiri kuona hatma ya kinda huyu anayesifiwa kwa uwezo mkubwa wa kufunga mabao, huku ikionekana kuwa Manchester United bado inaamini kuwa ni uwanja bora zaidi kwa ajili ya malezi yake ya soka.