Thomas Tuchel ashauriwa kumpa nafasi Will Lankshear badala ya Calvert-Lewin
Changamoto ya kuziba pengo la Harry Kane
Kocha wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel, amepata shinikizo kutoka kwa wadau wa soka wakimtaka kufikiria upya chaguo lake la mshambuliaji wa akiba kwa ajili ya nahodha Harry Kane. Inaonekana kuwa kuziba pengo la staa huyo wa Bayern Munich ni changamoto kubwa kwa soka la Uingereza kwa sasa, kwani hakuna mshambuliaji mwingine anayefikia kiwango chake.
Katika orodha ya hivi karibuni ya kikosi cha England, Tuchel alimjumuisha Dominic Calvert-Lewin kutoka Leeds United kama mbadala, lakini uteuzi huo umekumbwa na maneno kutoka kwa wachambuzi.
Maoni ya Troy Deeney
Mshambuliaji wa zamani wa Premier League, Troy Deeney, amekuwa wazi kabisa katika kukosoa uteuzi wa Calvert-Lewin. Akizungumza na talkSPORT, Deeney amedai kuwa mchezaji huyo hawezi kuwa jibu la kudumu kwa mustakabali wa England.
“Dominic Calvert-Lewin, kwa heshima zote, amefanya vizuri sana Leeds. Lakini wewe si jibu la matatizo yetu ya baadaye. Ninapendelea tuone sura mpya kama Will Lankshear. Huyu ni kijana ambaye anafunga mabao katika Championship, hebu tumlete tumwone kama anaweza kujifunza kutoka kwa Harry Kane na kuleta kitu cha tofauti kwa muda mrefu.”
Deeney anaamini kuwa badala ya kuendelea kuwaita wachezaji waliokwishaonekana uwezo wao kama ilivyokuwa kwa Ollie Watkins au Ivan Toney, ni vyema kocha akawapa fursa vijana wenye damu changa ili kupima uwezo wao wa kudumu kwenye timu ya taifa.
Will Lankshear anang’ara Middlesbrough
Will Lankshear, ambaye aliondoka Tottenham Hotspur msimu huu kujiunga na Middlesbrough kwa ada ya takriban £10 milioni, ameanza vyema msimu huu kwa kufunga mabao nane katika mechi 11 alizocheza. Kiwango hiki kimezua mjadala mkubwa, huku wachambuzi wengi wakiamini kuwa Tottenham walikosea kumuuza kijana huyo.
John Wenham, mtaalamu wa mambo ya Tottenham, anaona kuwa uamuzi wa kumuachia Lankshear ulikuwa ni kosa kubwa. Alisema:
“Inaonekana kama jambo la kipumbavu sana. Tumemuuza mshambuliaji ambaye ana ujasiri, ana umbo zuri la kuwa mshambuliaji, ni Mwingereza na anafunga mabao kwa urahisi. Hii si makosa tu, inaonekana kama maafa makubwa kwa klabu.”
Wakati Tuchel akiendelea kuijenga England, presha ya kutafuta mbadala sahihi wa Kane inaendelea kuongezeka. Swali kuu ni kama atamwamini kijana kama Lankshear katika dirisha lijalo la kimataifa au ataendelea na chaguo zake za sasa.