Roberto De Zerbi afunguka baada ya kichapo cha Tottenham: 'Tupo hatarini mno'
Kipigo kingine chaumiza Spurs
Kocha wa Tottenham, Roberto De Zerbi, amejikuta kwenye wakati mgumu baada ya timu yake kukubali kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya Aston Villa katika mchezo wa Ligi Kuu ya England (EPL) uliopigwa mwishoni mwa wiki hii. Matokeo haya yanaifanya Spurs kuingia kwenye mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa wakiwa katika eneo la hatari la kushuka daraja.
Licha ya Tottenham kuonekana kutawala mchezo na kutengeneza nafasi nyingi katika kipindi cha kwanza, walishindwa kuzitumia na kuadhibiwa na Johan Manzambi aliyewapa wageni bao la uongozi dakika za majeruhi kabla ya mapumziko. Katika kipindi cha pili, Nicolas Jackson na Emi Buendia waliongeza mabao mengine, huku jitihada za Conor Gallagher na Jan Paul van Hecke za kufunga mabao mawili ya kuchelewa zikishindwa kuwapa vijana wa De Zerbi walau pointi moja.
‘Tupo hatarini mno’
Akizungumza baada ya mchezo huo, De Zerbi hakuficha hisia zake juu ya udhaifu ulioonekana ndani ya kikosi chake, akisisitiza kuwa wachezaji wake hawana utulivu na nguvu ya kutosha kwenye vipindi muhimu vya mchezo.
“Nafikiri tulitakiwa kufunga mabao mengi sana kipindi cha kwanza. Tulifungwa wakati tukiwa tumebaki wachezaji 10, lakini tulitakiwa kuwa makini zaidi kwenye ulinzi. Katika kipindi cha pili, tumefungwa bao moja kwa moja kutoka kwenye mpira wa kipa. Tunatengeneza nafasi nyingi lakini sisi ni dhaifu mno,” alisema De Zerbi.
Kocha huyo raia wa Italia aliongeza kuwa anabeba lawama zote za matokeo haya mabaya, akisema kuwa soka linahitaji uthabiti ambao kikosi chake kimeshindwa kuuuonyesha.
Presha ya kufukuzwa inazidi kupanda
Kipigo hiki kimeongeza shinikizo kubwa kwa uongozi wa Tottenham, hususan kwa mashabiki ambao wameanza kupaza sauti zao kwenye mitandao ya kijamii wakitaka kocha huyo aondoke. Hali hii inazua mjadala mzito ikizingatiwa kuwa klabu hiyo ilitumia zaidi ya Pauni milioni 300 katika dirisha la usajili lililopita kwa lengo la kuboresha kikosi hicho.
Alipoulizwa kama mapumziko ya kimataifa yamekuja wakati sahihi, De Zerbi alionekana kutokuwa na uhakika:
“Sijui kama ni sahihi au la. Ni vigumu kutoa maoni kwa sababu tulicheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi. Ni ajabu jinsi mchezo unavyoweza kubadilika. Kuna kazi kubwa ya kufanya, na ni wajibu wangu kuhakikisha tunarekebisha haya,” aliongeza kocha huyo.
Kwa sasa, Spurs inakabiliwa na kibarua kigumu cha kujenga upya hali ya kujiamini kwa wachezaji wake, huku De Zerbi akijaribu kuleta nidhamu ya kiulinzi ambayo anaamini ndiyo itawasaidia kurudi kwenye mstari wa ushindi baada ya mapumziko.