Fabrizio Romano afunguka: Tottenham hawana mpango na Rafael Leao
Tottenham waelekeza nguvu kwingine
Katika hali ya kuondoa utata wa uvumi unaoendelea sokoni, mtaalamu wa masuala ya usajili Fabrizio Romano amekanusha taarifa zinazodai kuwa Tottenham Hotspur wapo kwenye mazungumzo na winga wa AC Milan, Rafael Leao.
Licha ya kuwepo kwa minong’ono mingi, Romano amesisitiza kuwa kwa sasa uongozi wa Spurs haujajihusisha na mchakato wowote wa kutaka kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno.
Walengwa wakuu ni kina nani?
Tottenham wanaonekana kuwa na vipaumbele vingine katika harakati zao za kuimarisha safu ya ushambuliaji baada ya kufanya usajili mkubwa katika maeneo ya ulinzi na kiungo hapo awali. Kwa mujibu wa Romano, macho ya klabu hiyo yameelekezwa kwa wachezaji wengine wawili wa Ligi Kuu ya England.
“Guys, my understanding is the main names to take into consideration for Tottenham for the winger positions are: Cody Gakpo – lakini kwa sasa Liverpool hawajafungua mlango wa kumuuza – na Savinho. Savinho ni ‘top target’ kwa Tottenham. Hawa wachezaji wawili ndio vipaumbele vyao kwa nafasi ya winga,” alisema Romano.
Romano aliongeza kuwa Savinho amekuwa akifuatiliwa na Spurs kwa muda mrefu, hata kabla ya dirisha hili la usajili kufunguliwa, huku kwa upande wa Cody Gakpo, bado kuna changamoto ya Liverpool kutokuwa tayari kumwachia mchezaji huyo kwa sasa.
Leao anataka changamoto mpya
Habari za Leao kutamani kucheza Ligi Kuu ya England zimekuwa zikivuma kwa muda, huku wachambuzi kama Andy Brassell wakiamini kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 anaweza kuwa chaguo bora kwa timu yoyote inayohitaji kasi na uwezo wa kubadili matokeo.
Brassell alibainisha kuwa ingawa kiwango cha Leao kimeonekana kushuka kidogo msimu uliopita kutokana na changamoto binafsi, bado ana ubora wa hali ya juu wa kucheza pembeni, akimfananisha na uwezo ambao uliwahi kuonekana kwa Heung-min Son kipindi cha nyuma.
“Kama Tottenham watafanikiwa kupata mchezaji mwenye uwezo wa kulipuka kama yeye, itakuwa ni nyongeza kubwa sana kwenye safu yao ya ushambuliaji. Anaweza kucheza pembeni na pia akawa tishio anapokatiza katikati,” aliongeza Brassell.
Hata hivyo, hadi sasa ni wazi kuwa Tottenham wamejikita zaidi katika mipango yao mingine, na Leao hatarajiwi kutua London Kaskazini katika dirisha hili.