Tottenham yajipanga kwa Top Four, nyota wanne watajwa kuwa nguzo muhimu
Tottenham kurejea kwenye ushindani wa nne bora
Baada ya kupita katika misimu miwili migumu ambapo klabu hiyo ilijikuta ikipambana kuepuka kushuka daraja, matumaini mapya yameanza kuchipuka ndani ya Tottenham Hotspur. Mchambuzi wa masuala ya klabu hiyo, John Wenham, anaamini kuwa kikosi hicho kina kila sababu ya kuweka malengo ya kumaliza kwenye nne bora (Top Four) msimu ujao.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Roberto De Zerbi, ambaye aliingia katika mechi saba za mwisho za msimu uliopita na kushinda tatu, yameleta sura mpya. Klabu tayari imeshamaliza asilimia 60 ya usajili wao wa majira ya kiangazi, ikiwa imesajili wachezaji sita wapya na sasa nguvu imeelekezwa katika safu ya ushambuliaji.
Nyota wanne ni muhimu kwa mafanikio
Licha ya usajili unaoendelea, Wenham anaamini kuwa wachezaji waliopo ambao walikosa mechi nyingi msimu uliopita ndio watakaokuwa nguzo ya mabadiliko hayo. Mchezaji anayetajwa kuwa na umuhimu mkubwa ni Mohammed Kudus.
“Kudus alikuwa mchezaji wetu bora msimu uliopita hadi alipoumia Januari. De Zerbi alimweleza jinsi anavyomtegemea, lakini majeraha yalikuwa pigo kubwa. Kumrejesha uwanjani ni sawa na kusajili mchezaji mpya,” alisema Wenham.
Hata hivyo, kuna wasiwasi juu ya afya ya nyota huyo ambaye amebaki kufanya mazoezi ya kuimarisha mwili badala ya kushiriki ziara ya maandalizi ya msimu (pre-season). Umahiri wake katika winga ya kulia unatajwa kuwa na mchango mkubwa chini ya mifumo ya De Zerbi, akifananishwa na jinsi kocha huyo alivyomtumia Kaoru Mitoma alipokuwa Brighton.
Matumaini ya safu ya ushambuliaji
Mbali na Kudus, Wenham anataja majina ya James Maddison, Xavi Simons, na Dejan Kulusevski kama wachezaji muhimu ambao, wakiwa fiti na katika kiwango bora, wana uwezo wa kuibeba Tottenham kuelekea kwenye nne bora.
Kwa upande wake, Roberto De Zerbi amekuwa wazi kuhusu mipango yake ya usajili. Kocha huyo amedokeza kuwa bado hajamaliza kazi yake kwenye soko la usajili.
“Kwenye soko la usajili, ninapomhitaji mchezaji, mimi huwa kama papa; hakuna nafasi ya kusema hapana! Soko halijafungwa, tumekamilisha asilimia 60 ya mradi wetu, sasa tunakuja na kitu kingine kikubwa (bomba),” alisema De Zerbi.
Mashabiki wa Spurs sasa wana kila sababu ya kutazama mbele kwa matumaini, wakiamini kuwa kwa mchanganyiko wa wachezaji waliopo na maboresho yanayofanywa na De Zerbi, klabu hiyo inaweza kurejea katika nafasi zake za awali kwenye Ligi Kuu ya Uingereza.