Skip to content

Tottenham yafukuzia saini ya Savinho kutoka Manchester City

SokaNews
Updated: Published: Jumamosi, 25 Julai 2026 · 2 min read
tottenham manchestercity savinho robertodezerbi usajili premierleague
Tottenham yafukuzia saini ya Savinho kutoka Manchester City

Tottenham bado wanamnyatia Savinho

Klabu ya Tottenham Hotspur inaendelea kufanya kazi kubwa katika dirisha hili la usajili huku mtaalamu wa masuala ya uhamisho, Fabrizio Romano, akithibitisha kuwa klabu hiyo ipo katika mazungumzo ya kumsajili winga wa Manchester City, Savinho.

Baada ya kufanya marekebisho makubwa katika safu ya kiungo kwa kuwasajili nyota kama Sandro Tonali na Mateus Fernandes, sasa kocha Roberto De Zerbi amegeuzia macho yake kwenye safu ya ushambuliaji. De Zerbi anataka kuongeza nguvu na ubora wa kipekee katika kikosi chake ili kiweze kushindana vyema msimu ujao.

Uamuzi mikononi mwa Man City

Tottenham walikuwa wakimfukuzia mchezaji huyu tangu msimu wa 2025, na inaonekana hamu hiyo haijapungua hata kidogo. Hata hivyo, dili hili linategemea kiasi kikubwa maamuzi ya Manchester City. Kulingana na Romano, mazungumzo kati ya pande zote mbili yanaendelea vyema.

“Tottenham bado wanavutiwa sana na Savinho. Wanaendelea kufanya kazi kwenye dili hilo. Wanasubiri Manchester City wafanye maamuzi kama wako tayari kumwachia mchezaji huyo na kwa masharti yapi. Lakini mazungumzo yameanza na yanaendelea.”

Romano aliongeza kuwa De Zerbi ameweka wazi mahitaji yake kwa uongozi wa Spurs:

“Kocha Roberto De Zerbi alisema baada ya kuimarisha kiungo na ulinzi, sasa wanahitaji kufanya kitu mbele. Wanahitaji wachezaji muhimu, si wachezaji wa kawaida tu. Na anaposema hivyo, anamaanisha Savinho ni mmoja wa wachezaji wanaomtaka kwa dhati.”

Safari ya usajili inaendelea

Inaripotiwa kuwa gharama ya kumsajili winga huyo wa Kibrazil inaweza kufikia paundi milioni 60. Tottenham wapo tayari kupambana ili kumnasa, ingawa kwa sasa wanasubiri ‘taa ya kijani’ kutoka Etihad Stadium. Manchester City inaweza kusubiri kwanza kumpata mbadala wake kabla ya kuruhusu dili hilo kukamilika.

Licha ya Savinho kuwa mlengwa mkuu, inasemekana kuwa Tottenham pia wanatazama uwezekano wa kumsajili Cody Gakpo kama mbadala mwingine wa kuimarisha nafasi za pembeni. Kwa sasa, mashabiki wa Spurs wanasubiri kuona hatma ya dili hili ambalo linaonekana kuwa “lipo mezani” na lina kila dalili ya kufanikiwa.