Skip to content

Tottenham yafukuzia saini ya Arne Engels, Vicario kutimka?

SokaNews
Updated: Published: Jumatatu, 20 Julai 2026 · 2 min read
tottenham celtic usajili arneengels guglielmovicario
Tottenham yafukuzia saini ya Arne Engels, Vicario kutimka?

Tottenham yatinga sokoni tena

Klabu ya Tottenham Hotspur inaonekana kutotaka kurudia makosa ya msimu uliopita, ambapo walinusurika kushuka daraja katika dakika za mwisho za ligi. Chini ya kocha Robert De Zerbi, Spurs wameanza mchakato wa kuboresha kikosi chao kwa kasi kubwa, wakiwa tayari wameshasajili wachezaji sita wapya.

Ripoti mpya kutoka Uingereza zinaeleza kuwa Tottenham imejitokeza kama klabu ya hivi karibuni kuanza kufuatilia saini ya kiungo wa Celtic, Arne Engels. Hatua hii imewashangaza wengi kutokana na ukweli kwamba Spurs tayari wameshajipatia huduma za viungo wengine kama Sandro Tonali na Mateus Fernandes katika dirisha hili la usajili.

Engels anavutika na Premier League

Mwandishi wa habari za michezo, Pete O’Rourke, amedokeza kuwa inaweza kuwa vigumu kwa Celtic kumbakiza mchezaji huyo, hasa baada ya ofa ya awali kukataliwa Januari iliyopita. Licha ya kufanikiwa kuingiza nyuso mpya kwenye safu ya kiungo, Spurs wanaonekana hawana mpango wa kusimama.

“Nina hakika Engels mwenyewe angevutiwa na fursa ya kuondoka ikiwa ofa kutoka Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League) itakuja. Kwa upande wa Tottenham, nia yao inashangaza kidogo kutokana na maboresho waliyokwisha yafanya kwenye eneo la kiungo,” alisema O’Rourke.

Mabadiliko kwenye lango la Spurs

Wakati kiungo huyo akiwa kwenye rada za Tottenham, hali ya kipa wao, Guglielmo Vicario, inaonekana kuwa shakani. Vicario, ambaye alikuwa na msimu mgumu kikosini hapo, anatajwa kuwa njiani kuondoka kufuatia tetesi za kubadilishwa na kipa wa Napoli, Vanja Milinković-Savić.

Vyombo vya habari nchini Italia vimeripoti kuwa kuna uwezekano wa kufanyika kwa dili la kubadilishana wachezaji (swap deal), ambapo Vicario angeelekea Italia na Milinković-Savić akija London. Thamani za wachezaji hao wawili zinaelezwa kuwa karibu, jambo linalofanya mazungumzo hayo kuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa.

Mtaalamu wa masuala ya uhamisho, Fabrizio Romano, hapo awali alithibitisha kuwa Vicario huenda akaondoka Tottenham, huku vilabu kadhaa vya Italia vikiwa vimeonyesha nia ya kumnyakua. Napoli imekuwa ikifuatilia hali hiyo kwa karibu sana, ikijipanga kumpata kipa huyo endapo watapata mnunuzi wa mlinda mlango wao wa sasa.

Hadi sasa, Tottenham inaendelea kuwa busy sokoni huku lengo lao kuu likiwa ni kujenga kikosi imara kitakachoweza kuhimili mikikimikiki ya msimu ujao bila wasiwasi wa kushuka daraja tena.