Thomas Tuchel afunguka kuhusu kauli ya Jude Bellingham baada ya ushindi dhidi ya Norway
Ujumbe wa Tuchel kwa Bellingham
Kocha mkuu wa England, Thomas Tuchel, ameweka wazi msimamo wake baada ya kuibuka kwa mvutano mdogo wa maneno baina yake na nyota wa timu hiyo, Jude Bellingham, kufuatia ushindi wa 2-1 dhidi ya Norway katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia.
Baada ya mchezo huo mgumu ambapo England walilazimika kupindua matokeo, Bellingham, ambaye alifunga mabao yote mawili, alionekana kutofautiana na mtazamo wa kocha wake kuhusu kiwango cha timu. Wakati akihojiwa, Bellingham alisisitiza kuwa wachezaji walifanya kazi kubwa na kuonyesha juhudi za hali ya juu uwanjani.
“Oh well, vyovyote ilivyo… ni ngumu sana kule uwanjani. Ni kazi nzito. Wachezaji wote walifanya kazi nzito sana. Hivyo, mawazo yangu na shukrani zangu zinaenda kwa wachezaji waliojituma na kufanya kazi kubwa kwa mara nyingine tena,” alisema Bellingham mara baada ya mchezo.
Tuchel hakubaliani na kiwango cha soka
Katika mkutano na wanahabari, Tuchel alijikuta akijibu swali kuhusu kauli hiyo ya staa wake. Licha ya kukiri kuwa anaheshimu juhudi za wachezaji wake, kocha huyo Mjerumani alisisitiza kuwa bado kuna nafasi kubwa ya kuboresha soka lao.
“Kabisa, hakuna anayepinga hilo. Nimevutiwa na juhudi walizozionyesha, morali ya timu na imani. Kushinda wakati unapopitia changamoto ni jambo la kiwango cha juu sana. Hawatakiwi kukosa sifa kwa hilo,” alisema Tuchel.
Hata hivyo, aliongeza:
“Lakini mimi ni kocha wa soka, na nadhani tunaweza kucheza vizuri zaidi. Kwa ujumla, huu haukuwa mchezo wa kiwango cha juu. Akili yangu ya kocha bado inaamini kuwa tunaweza na tunapaswa kucheza soka bora zaidi.”
Utegemezi kwa Bellingham na Kane
Katika michuano hii, Jude Bellingham na Harry Kane wamekuwa nguzo kuu, wakifunga mabao 12 kati ya 13 yaliyofungwa na England. Tuchel anakiri kuwa anahitaji kuona wachezaji wengine wakijitokeza, lakini hawezi kulalamikia ubora wa wawili hao.
“Tunahitaji kuboreka kwenye eneo la ushambuliaji ili kuwaweka wachezaji wengine kwenye nafasi nzuri pia. Lakini bila shaka, hawa ni wachezaji wa maamuzi. Wanapenda majukumu na wana ubora. Hakuna kibaya kwao kufanya hivyo na hatuhitaji kuomba radhi kwa sababu wao wapo kwetu,” aliongeza Tuchel.
England sasa inajiandaa kwa mchezo ujao wa nusu fainali utakaopigwa Atlanta siku ya Jumatano, ambapo watakutana na mshindi kati ya Argentina na Uswisi.