Mgogoro FIFA: UEFA yamtolea uvivu Infantino, yasisitiza kutokuwa na imani naye
Mgogoro wa Uongozi waendelea kufukuta
Uhusiano kati ya Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA) na Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, unazidi kuwa mbaya. Hii ni baada ya UEFA kusisitiza kuwa msamaha uliotolewa na Infantino kufuatia mpango wake wa kibiashara uliozua utata, hauna maana yoyote kwao.
Awali, Infantino alipanga kuuza sehemu ya FIFA kupitia kampuni iliyofahamika kama ‘FIFA Forward Enterprise’ (FFE), hatua ambayo ingewapa mamlaka ya kuendesha mashindano makubwa kama Kombe la Dunia. Mpango huu ulipingwa vikali duniani kote, jambo lililomlazimu Infantino kufuta wazo hilo siku chache baadaye.
Msamaha uliokaliwa kikaoni
Katika jaribio la kutuliza joto, Infantino alitoa taarifa ya kuomba radhi akisema:
“Tunakubali kuwa kulikuwa na makosa katika mchakato wa uanzishwaji wa FIFA Forward Enterprise (FFE). Hatukuwa na nia ya kuwatenga wajumbe wa Baraza la FIFA na vyama wanachama, na jambo hili lilipaswa kushughulikiwa kwa namna tofauti. Tunaomba radhi kwa makosa haya na tunaahidi kutoyarudia.”
Hata hivyo, UEFA imejibu mapigo kwa kusema kuwa msamaha huo umechelewa na hauzingatii matakwa yao ya msingi. Katika taarifa yao kali, UEFA ilisisitiza kuwa bado hawana imani na uongozi wa Infantino.
UEFA yaweka msimamo wazi
UEFA imesema kuwa masharti yao ya awali hayajatekelezwa. Wanachama wa UEFA walikuwa wameweka wazi kuwa ili kurejesha mahusiano, ni lazima mipango ya kuuza mashindano ifutwe na wawekewe hakikisho kuwa vitendo vya namna hiyo havitajirudia tena.
“Taarifa ya jana kwamba baadhi ya watu walioajiriwa na rais wa FIFA wanakubaliana naye, haibadilishi chochote. Msimamo wetu wa kupoteza imani na uongozi wa Gianni Infantino unabaki pale pale,” ilisema taarifa ya UEFA.
Hatima ya Infantino mashakani
Kutokana na hali hii, kuna tishio kubwa la nchi za Ulaya kususia mashindano yajayo ya FIFA ikiwa Infantino ataendelea kusalia madarakani. Hii ni pigo kubwa kwa Infantino ambaye anatarajia kugombea muhula wa nne katika uchaguzi utakaofanyika Machi 2027.
Ili kushinda, mgombea anahitaji angalau kura 106 kati ya wanachama 211. Kwa kupoteza kura 55 za mataifa ya Ulaya, na huku baadhi ya nchi nyingine zikionekana kumuunga mkono UEFA, ndoto ya Infantino ya kuendelea kuongoza FIFA inaonekana kuwa katika wakati mgumu sana.