Guglielmo Vicario aaga Tottenham, kujiunga na Juventus
Vicario arejea Italia
Klabu ya Tottenham Hotspur imethibitisha kukubaliana na Juventus kwa ajili ya uhamisho wa kipa wao, Guglielmo Vicario. Mtaalamu wa masuala ya usajili barani Ulaya, Fabrizio Romano, ametoa uthibitisho wake wa ‘here we go’, akionyesha kuwa makubaliano yameshafikiwa na kipa huyo anaondoka jijini London kurejea nchini Italia.
Uhamisho huu umekuja baada ya majadiliano ya muda mfupi kati ya klabu hizo mbili, ambapo Juventus walikuwa wakimtafuta kipa mpya baada ya mpango wao wa kumsajili Emiliano Martinez kutoka Aston Villa kushindikana.
Maelezo ya dili hilo
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Romano na mwandishi nguli David Ornstein, dili hilo ni la mkopo wa msimu mmoja wenye kipengele cha Juventus kuwa na chaguo la kumnunua moja kwa moja kipa huyo mwenye umri wa miaka 29 mwisho wa msimu.
“Juventus wamekubaliana kumsajili Guglielmo Vicario kutoka Tottenham, here we go! Spurs wamekubali ofa ya mkopo na kipengele cha kununua - si lazima. Vicario alitaka uhamisho huu na anaondoka Spurs leo,” alieleza Romano kupitia ukurasa wake wa X.
Safari ya Vicario kuelekea Turin
Vicario alikuwa na kipindi kigumu mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kufanyiwa upasuaji wa ngiri (hernia) mwezi Machi. Nafasi yake ilichukuliwa na Antonin Kinsky, na tangu hapo ilionekana wazi kuwa mlinda mlango huyo wa Italia alikuwa akielekea ukingoni mwa maisha yake klabuni hapo.
Inaripotiwa kuwa wakala wa mchezaji huyo alikuwa jijini Turin kwa ajili ya masuala mengine ya usajili, jambo lililorahisisha mazungumzo kati yake na uongozi wa Juventus kukamilisha dili hilo kwa haraka.
Kwa upande wa Juventus, huu ni uimarishaji muhimu wa kikosi chao kwa ajili ya changamoto za Serie A msimu huu, huku Tottenham wakitarajiwa kuendelea na mipango mingine ya usajili baada ya kumwachia Vicario ambaye alionyesha nia ya kutaka kurejea nyumbani Italia.