Vinicius Junior kubaki Real Madrid: Arsenal wamepigwa kumbo na ofa mpya
Matumaini ya Arsenal kutua kwa Vinicius yafutika
Ndoto za mashabiki wa Arsenal kumuona staa wa Real Madrid, Vinicius Junior, akitua uwanjani Emirates zinaelekea kufika ukingoni. Mtaalamu wa masuala ya usajili barani Ulaya, Fabrizio Romano, ametoa taarifa inayowapa ahueni mabingwa hao wa Hispania huku ikiiacha Arsenal bila majibu ya kuridhisha.
Kumekuwa na tetesi nyingi katika siku za hivi karibuni zikidai kuwa nyota huyo wa Kibrazili huenda akaondoka Santiago Bernabeu ili kuanza changamoto mpya jijini London. Hata hivyo, hali ya hewa imeanza kubadilika baada ya mazungumzo ya ana kwa ana kati ya mchezaji huyo, mawakala wake kutoka Roc Nation, na uongozi wa Real Madrid.
Ofa nono yabadili mwelekeo
Awali, Vinicius alikuwa amegoma kusaini ofa kadhaa zilizowasilishwa na Madrid, akihisi malipo hayo hayakidhi hadhi yake kama mmoja wa wachezaji bora duniani kwa sasa. Hali hiyo iliwapa Arsenal mwanya wa kuingilia kati, ambapo waliripotiwa kufikia mahitaji ya mshahara ya mchezaji huyo.
Lakini, Fabrizio Romano amebainisha kuwa Real Madrid wameongeza dau lao kwenye mkataba mpya ili kumshawishi mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26.
“Uelewa wangu ni kwamba baada ya kikao cha ana kwa ana leo huko Madrid, makubaliano ya Vinicius Junior kusalia Real Madrid na kusaini mkataba mpya yamefikia hatua nzuri sana,” alisema Romano kwenye ukurasa wake wa YouTube.
Uamuzi wa mwisho kusubiriwa
Ingawa bado hakujawa na tamko rasmi la Vinicius kukubali ofa hiyo, Romano anaamini kuwa ni suala la muda tu. Real Madrid wanataka kupata jibu la mwisho kutoka kwa staa huyo ndani ya saa chache zijazo ili kumaliza sakata hilo ambalo limekuwa likitafuna vichwa vya wadau wa soka kwa miezi 18 sasa.
Kwa upande wake, mwandishi mashuhuri David Ornstein amethibitisha kuwa Arsenal walikuwa wamejipanga vilivyo kumnasa mchezaji huyo kwa kuweka ‘kila kitu’ mezani. Hata hivyo, hatua ya Madrid kuongeza ofa inayozingatia umuhimu wa Vinicius katika mradi wao wa soka imeonekana kuwa kikwazo kikubwa kwa Gunners.
Kwa sasa, ni wazi kuwa Vinicius anaelekea kusalia Madrid, jambo ambalo linamaanisha Mikel Arteta na kikosi chake watalazimika kuelekeza nguvu zao kwenye malengo mengine katika dirisha hili la usajili.