Hatima ya Vinicius Junior Real Madrid: Arsenal wamekaa mkao wa kula
Vinicius Junior na mchakato wa kusalia Bernabeu
Mshambuliaji nyota wa Real Madrid, Vinicius Junior, anarejea jijini Madrid wiki hii kwa ajili ya mazungumzo mapya ya mkataba na uongozi wa klabu hiyo. Licha ya kuwepo kwa tetesi nyingi zinazomhusisha na klabu ya Arsenal, vyanzo vya karibu vinaeleza kuwa kipaumbele cha Mbrazil huyo bado ni kuendelea kusalia katika viunga vya Santiago Bernabeu.
Hata hivyo, mazungumzo hayo yanaonekana kuwa na changamoto. Ingawa pande zote mbili zimekubaliana kuhusu mshahara na muda wa mkataba, kuna mvutano mkubwa kuhusu bonasi ya usajili ambayo Vinicius anaitaka. Kwa sasa, hii ndiyo kikwazo kikubwa ambacho kinaweza kusababisha mpango huo kukwama ikiwa pande zote hazitakuwa tayari kulegeza msimamo.
Arsenal wapo vitani
Wakati hali ikiwa tete Madrid, Arsenal wameendelea kuonyesha nia ya dhati ya kumsajili staa huyo. Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, inaelezwa kuwa tayari amezungumza na mchezaji huyo ili kumweleza ramani yake na umuhimu wa Vinicius katika kukuza zaidi mradi wa Arsenal kufuatia mafanikio yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu uliopita.
Arsenal wanaonekana kutaka kuimarisha kikosi chao kwa wachezaji wenye ubora wa hali ya juu. Baada ya kumsajili kipa Illan Meslier na mshambuliaji Christos Tzolis, pamoja na kumfanya Piero Hincapie kuwa mchezaji wa kudumu, mabingwa hao wa EPL wanajipanga kufanya usajili mkubwa utakaotikisa soka la dunia.
Je, ni usajili wa kihistoria?
Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Everton, Keith Wyness, anaamini kuwa ikiwa Arsenal watafanikiwa kuinasa saini ya Vinicius, itakuwa ni ishara kubwa ya nia yao ya kutawala soka la Uingereza na Ulaya. Wyness anaamini kuwa kuja kwa mchezaji wa aina ya Vinicius kutasaidia kuongeza thamani ya Ligi Kuu ya England kimataifa.
“Itakuwa vizuri kuona mchezaji mwenye kipaji kama hicho akicheza Ligi Kuu ya England. Itakuwa ni usajili wa kihistoria ambao utabadilisha taswira ya timu na kuonyesha dhamira kubwa ya Arsenal,” alisema Wyness.
Hata hivyo, inaaminika kuwa Arsenal watalazimika kuuza baadhi ya wachezaji wao ili kuwezesha usajili wa aina hiyo na kufuata kanuni za matumizi ya fedha. Kwa sasa, macho yote yanaelekezwa wiki hii ambapo Vinicius anatarajiwa kuuweka wazi msimamo wake mbele ya viongozi wa Real Madrid.