Wachezaji wa Hispania wameweka wazi timu wanayotamani kukutana nayo fainali ya Kombe la Dunia
Hispania watinga fainali kwa kishindo
Timu ya taifa ya Hispania imethibitisha ubora wake baada ya kufanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Dunia kufuatia ushindi wa bao 2-0 dhidi ya Ufaransa katika mchezo wa nusu fainali. Vijana hawa wa Luis de la Fuente, ambao pia ndio mabingwa wa Euro 2024, walionyesha kiwango cha juu na kuwazidi maarifa wakali hao wa soka duniani, Ufaransa.
Wakati Hispania wakisubiri mpinzani wao katika mchezo wa fainali, macho yote sasa yameelekezwa katika nusu fainali nyingine inayozikutanisha England na Argentina. Hata hivyo, imebainika kuwa kikosi cha Hispania tayari kina matamanio yao kuhusu nani anayepaswa kuwa mpinzani wao katika mchezo huo wa mwisho.
Tamaa ya kukutana na Argentina
Kulingana na ripoti za mwandishi wa habari za michezo kutoka Uhispania, Juanfe Sanz, wachezaji wa timu hiyo ya taifa wana hamu kubwa ya kukutana na Argentina kuliko England.
“Ni dhahiri kabisa kwamba katika vyumba vya kubadilishia nguo vya Hispania, timu ambayo wachezaji wanatamani kukutana nayo ni Argentina. Hawataka fainali dhidi ya England, wanataka Argentina,” alisema Sanz.
Kwa nini wanataka Argentina?
Sanz ameeleza kuwa kuna mambo mengi yanayochochea hamu hiyo ya wachezaji wa Hispania. Anaeleza kuwa ni kutokana na aina ya kejeli wanazozipata kutoka kwa baadhi ya vyombo vya habari vya Argentina, pamoja na kumbukumbu ya mchezo wa kirafiki (Finalissima) uliopangwa kufanyika awali lakini ukashindikana, jambo ambalo lilileta maneno mengi kutoka kwa wapinzani hao.
“Ni dhoruba kamili. Kuna taarifa ambazo zimefika kwenye kambi ya timu, jinsi baadhi ya vyombo vya habari vya Argentina vimekuwa vikitudharau na kusema wao ndio mabingwa wa Kombe la Dunia hata kabla ya muda. Sasa muda umefika wa kuthibitisha uwanjani,” aliongeza mwandishi huyo.
Hata hivyo, Hispania sasa wanabaki kuwa watazamaji huku wakisubiri mshindi kati ya England na Argentina, wakiwa na imani kubwa na kikosi chao ambacho kimekuwa kikitamba kwa soka la kuvutia na kujiamini kupita kiasi katika mashindano haya ya mwaka 2026.