Wayne Rooney amuomba radhi Benjamin Sesko baada ya kumkosoa
Rooney ajirekebisha baada ya kumshambulia Sesko
Gwiji wa Manchester United, Wayne Rooney, amejikuta akilazimika kuomba radhi kwa mshambuliaji wa sasa wa klabu hiyo, Benjamin Sesko, baada ya kuibuka kwa taarifa za kweli kuhusu jeraha linalomkabili mchezaji huyo. Awali, Rooney alikuwa miongoni mwa watu waliohoji nia ya Sesko ya kutocheza akidai jeraha la mguu (shin injury) si kisingizio cha kukosa mechi muhimu.
Katika maoni yake yaliyozua mjadala wiki iliyopita, Rooney alikosoa hali ya mshambuliaji huyo akidai kuwa mchezaji anayeichezea klabu kubwa kama Manchester United anapaswa kucheza hata kama ana maumivu, akitoa mfano wa jinsi wachezaji wa zamani walivyokuwa wakitumia sindano ili kukazana uwanjani.
Ukweli wa jeraha la Sesko
Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kina, imebainika kuwa Sesko, aliyesajiliwa kwa kitita cha pauni milioni 73.7 kutoka RB Leipzig msimu uliopita, anasumbuliwa na jeraha la muda mrefu katika mguu wake. Hali hiyo imemfanya mshambuliaji huyo raia wa Slovenia kukosa hata michezo ya timu yake ya taifa katika dirisha hili la kimataifa.
Baada ya kupata taarifa hizo, Rooney hakusita kuonyesha uungwana na kumtaka radhi mchezaji huyo kupitia kipindi cha The United Stand.
“Kama ni jeraha la muda mrefu, basi nadhani ninapaswa kuomba radhi. Kwa hiyo, nakuomba radhi Sesko. Naomba radhi ikiwa nimekukosea na kukuhukumu vibaya. Samahani.”
Shinikizo la wachezaji wa zamani
Kabla ya Rooney kuomba radhi, wachezaji wengine wa zamani wa United kama Paul Scholes na Nicky Butt nao walikuwa wamemkosoa vikali Sesko. Scholes alihoji kama jeraha hilo ni la kuvunjika mfupa, huku Butt akieleza kushangazwa na United kuwa na mshambuliaji mmoja pekee ambaye naye anasumbuliwa na maumivu ya mguu.
Kwa sasa, Manchester United bado hawajatoa taarifa rasmi kuhusu muda kamili ambao Sesko atakuwa nje ya uwanja, jambo ambalo ni pigo kubwa kwa kocha na mashabiki wa klabu hiyo ambao wamekuwa wakimtegemea kijana huyo kama tegemeo lao kuu katika safu ya ushambuliaji.