Yan Diomande aipa pigo Liverpool baada ya kufichua 'mapenzi ya dhati' kwa PSG
Mbio za kumsaka mshambuliaji hatari wa RB Leipzig, Yan Diomande, zimechukua sura mpya baada ya kinda huyo mwenye umri wa miaka 19 kuweka wazi hisia zake za dhati kwa miamba ya soka ya Ufaransa, Paris Saint-Germain (PSG). Hatua hii inatajwa kuwa pigo kubwa kwa majogoo wa Merseyside, Liverpool, ambao wamekuwa wakimtazama kijana huyo kama mrithi sahihi wa nguli wao, Mohamed Salah.
Diomande, ambaye kwa sasa yupo Amerika Kaskazini akijiandaa na fainali za Kombe la Dunia akiwa na timu ya taifa ya Ivory Coast, amekuwa gumzo kubwa barani Ulaya kutokana na kiwango chake bora msimu huu. Huku klabu yake ya Leipzig ikisita kumwachia, dau nono linalokadiriwa kufikia euro milioni 100 hadi milioni 150 linaweza kuwalainisha matajiri hao wa Ujerumani ili kumwachia nyota huyo.
Kauli ya Diomande Ilivyozua Taharuki Liverpool
Katika mahojiano yake na gazeti maarufu la nchini Ufaransa la L’Equipe kabla ya kuanza kwa kampeni ya Kombe la Dunia, winga huyo mwenye kasi ya hatari ametoa kauli iliyozima kwa kiasi kikubwa matumaini ya Liverpool kupata saini yake kwa urahisi.
Diomande alisema:
“Paris Saint-Germain ni timu ambayo nimeipenda tangu nikiwa mdogo. Baba yangu ni shabiki mkubwa wa Paris Saint-Germain, na ni timu ambayo ninaivunja nguvu na kuiheshimu sana kama shabiki wa soka. Ingekuwa furaha kubwa kwangu kwenda kucheza pale kwenye moja ya klabu kubwa zaidi duniani. Siku zote ni furaha kwenda pale kwa sababu lugha ya Kifaransa inazungumzwa, na nadhani kuzoea mazingira kusingekuwa kugumu sana. Lakini, kwa nini isiwezekane? Sifikirii sana kuhusu mustakabali wangu kwa sasa wala kujielekeza kwenye mambo mengine. Kama nilivyosema, kwa sasa nipo makini zaidi na Kombe la Dunia. Baada ya hapo, klabu zitamalizana zenyewe na tutaona kitakachofuata.”
Dau la Leipzig na Vita ya Dau la Usajili
Taarifa kutoka nchini Ujerumani kupitia jarida la BILD zinasema kuwa Leipzig inaweza kung’ang’ania dau la hadi euro milioni 150 ili kumwachia lulu yao hiyo. Liverpool ipo tayari kufanya mazungumzo, na mwandishi wa habari za usajili Fabrizio Romano alifichua kuwa mchezaji huyo angependa dili lake likamilike mapema. Hata hivyo, PSG nao wanaamini kuwa Diomande anaweza kuongeza nguvu kubwa kwenye safu yao ya ushambuliaji ambayo tayari inatisha.
Mwandishi wa habari kutoka Ufaransa, Santi Aouna, amewahi kuripoti kuwa Diomande alikuwa ametoa ridhaa yake ya kujiunga na Liverpool na PSG, lakini kauli yake ya mwisho inaonyesha anaegemea zaidi kwa mabingwa hao wa Ufaransa.
Je, Matumaini ya Liverpool Yamekufa Kabisa?
Licha ya kauli hiyo inayokatisha tamaa kwa upande wa Anfield, bado kuna mwanga wa matumaini kwa upande wao. Ripoti kutoka FootMercato zinaeleza kuwa PSG wanasita kulipa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kinaweza kusababishwa na ushindani wa kupandisha bei (bidding war).
PSG wanaamini kuwa tayari wana kikosi chenye vipaji vya kutosha na hawana nia ya kutumia fedha vibaya kwa ajili ya mchezaji yeyote, hata kama Diomande ameeleza nia yake ya kujiunga nao. Taarifa ya FootMercato ilisema:
“Kulingana na vyanzo vyetu, Yan Diomande ametoa kibali chake kujiunga na Paris Saint-Germain. Hii ni hatua muhimu, kwani klabu ya Paris inasubiri kuona nia ya pande zote mbili kabla ya kuchukua hatua. Kwa upande mwingine, Diomande hana shauku kubwa ya kujiunga na Bayern Munich ambao nao wanamtaka. Hata hivyo, bado anavutiwa na nafasi ya kujiunga na Liverpool…”
Hii ina maana kuwa ikiwa PSG watashindwa kufikia makubaliano na Leipzig au wakajiondoa kwenye mbio hizo kutokana na bei kubwa, Liverpool watabaki kwenye nafasi nzuri ya kumsajili chini ya kocha wao mpya anayetarajiwa, Andoni Iraola.
Nini Kinafuata kwa Diomande?
Kwa sasa, macho yote yapo kwenye fainali za Kombe la Dunia. Kama Diomande ataonyesha kiwango kikubwa kwenye michuano hiyo, thamani yake inaweza kupaa hata zaidi ya kiwango kilichotajwa sasa, jambo ambalo linaweza kuzifanya klabu hizi mbili kufikiria mara mbili kuhusu uamuzi wao.
Mashabiki wa soka nchini Tanzania na kote duniani watasubiri kwa hamu kuona kama kijana huyu atakwenda kurithi mikoba ya Salah pale Anfield au atatua kujiunga na timu ya ndoto zake kule Paris.