Yan Diomande awapiga chenga Arsenal na Man City, Real Madrid yafukuzia saini yake
Real Madrid yafukuzia saini ya Diomande
Kinda wa kimataifa wa Ivory Coast, Yan Diomande, amekuwa gumzo katika dirisha hili la usajili huku klabu kubwa za Ulaya zikipambana kumnasa kutoka RB Leipzig. Habari za hivi punde kutoka kwa mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, zinaonyesha kuwa kinda huyo mwenye umri wa miaka 19 amegomea ofa za kujiunga na vigogo wa Ligi Kuu ya England, Arsenal na Manchester City.
Licha ya klabu hizo mbili za jijini London na Manchester kufanya mawasiliano na watu wa karibu na mchezaji huyo ndani ya siku kumi zilizopita, Diomande ameonekana kutokuwa na nia ya kuhamia nchini England. Romano amethibitisha kuwa mchezaji huyo hakufungua milango ya mazungumzo na klabu yoyote ya Ligi Kuu ya Uingereza (PL).
Makubaliano na Real Madrid
Kwa sasa, Real Madrid inaonekana kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kumsajili staa huyo. Inafahamika kuwa klabu hiyo ya Santiago Bernabeu imefikia makubaliano ya maneno na mchezaji mwenyewe kuhusu maslahi binafsi. Hii ni mara ya pili kwa mchezaji huyo kufikia makubaliano kama hayo, baada ya awali kufanya hivyo na Paris Saint-Germain (PSG) mwezi Juni.
“Manchester City na Arsenal walijaribu kufanya mawasiliano kwa ajili ya Yan Diomande ndani ya siku kumi zilizopita, lakini mchezaji hakufungua milango. Hakuna ofa zozote zilizotoka klabu za England, na Real Madrid ndiyo klabu inayopambana kikamilifu kuikabili PSG kwa sasa,” alisema Romano.
Vita vya ofa za mamilioni
Real Madrid tayari imewasilisha ofa ya kwanza ya Euro milioni 90 pamoja na nyongeza ya Euro milioni 10, hata hivyo RB Leipzig imekataa ofa hiyo. Inaripotiwa kuwa Madrid wanajiandaa kurejea na ofa nyingine iliyoboreshwa ili kuhakikisha wanakamilisha dili hilo.
Kwa upande mwingine, mwandishi wa Sky Sports, Philipp Hinze, amedokeza kuwa mkataba wa miaka mitano hadi 2031 tayari umeshapangwa mezani. Changamoto iliyobaki ni makubaliano ya ada ya uhamisho kati ya klabu hizo mbili.
Jambo moja kubwa linalozungumziwa ni ikiwa Diomande atajiunga na Real Madrid moja kwa moja msimu huu au atasajiliwa kisha kurudishwa kwa mkopo RB Leipzig kwa msimu wa 2026/27. Ada ya mwisho ya uhamisho inatarajiwa kutegemea sana uamuzi huo wa klabu husika, kwani uhamisho wa haraka unatajwa kuwa na gharama kubwa zaidi kuliko ule wa mkopo wa kurudi Leipzig.