Youri Tielemans kukamilisha usajili wake Manchester United, Joao Gomes anatajwa kuwa chaguo la tatu
Usajili wa Tielemans sasa ni rasmi
Klabu ya Manchester United imeendelea na harakati zao za kufanya maboresho makubwa katika eneo la kiungo kuelekea msimu ujao, baada ya mtaalamu wa masuala ya usajili barani Ulaya, Fabrizio Romano, kuthibitisha kuwa klabu hiyo imekamilisha vipimo vya afya vya nyota wa Aston Villa, Youri Tielemans.
Taarifa zinaeleza kuwa dili hilo sasa ni “done and sealed” (limekamilika na kufungwa), huku kiungo huyo wa kimataifa wa Ubelgiji akitarajiwa kusaini mkataba wa miaka mitano utakaomfanya kusalia Old Trafford hadi Juni 2031. Manchester United ililazimika kulipa ada ya pauni milioni 35 ili kuwasha kipengele cha kuvunja mkataba wake na Aston Villa.
Romano aliongeza kuwa mchezaji huyo tayari alishawasili jijini Manchester kwa ajili ya kukamilisha taratibu za mwisho za kuhamia klabuni hapo. Hii ni hatua nyingine muhimu kwa United baada ya hivi karibuni kukamilisha usajili wa Andrey Santos kutoka Chelsea kwa ada ya takriban pauni milioni 50.
United kutazama upya chaguo la tatu
Wakati Tielemans akitarajiwa kutangazwa rasmi, Manchester United inaonekana bado haijamaliza kazi katika eneo la kiungo. Ripoti kutoka Football Insider zinaeleza kuwa klabu hiyo sasa inaelekeza nguvu zao kwa kiungo wa Wolves, Joao Gomes, ili awe kiungo wa tatu kusajiliwa katika dirisha hili.
Gomes, mwenye umri wa miaka 25, anatajwa kuwa chaguo la muda mrefu la United na inaripotiwa kuwa Wolves wako tayari kumwachia kwa ada ya karibu pauni milioni 30 kufuatia klabu hiyo kushuka daraja hadi Championship.
Mipango ya muda mrefu ya INEOS
Uongozi wa United chini ya INEOS umeonekana kuwa na utaratibu wa kutaka kuleta viungo watatu wapya ili kuziba nafasi na kupunguza utegemezi kwa wachezaji wa zamani. Ingawa Manuel Ugarte anatarajiwa kubaki kikosini licha ya kupata jeraha kubwa wakati wa michuano ya Kombe la Dunia, hii haijazuia United kuendelea na mpango wao wa kusuka upya safu yao ya kiungo.
Imebainika pia kuwa dili la kumleta Ederson Silva kutoka Atalanta limefika mwisho na halitatokea tena, hali iliyoilazimu United kubadili muelekeo na kuwawinda wachezaji wengine kama Joao Gomes, ambaye alikuwa akihusishwa na Atletico Madrid hapo awali.
“Youri Tielemans amekamilisha vipimo vyake vya afya na anasaini mkataba wake leo Manchester United. Mkataba utakuwa wa miaka mitano, hadi Juni 2031. Kila kitu kimekamilika,” alithibitisha Romano kupitia mitandao yake ya kijamii.