Arsenal yajipanga kunasa saini ya Morgan Rogers kwa kitita cha pauni milioni 80
Arsenal wamepania kuongeza nguvu safu yao ya ushambuliaji
Klabu ya Arsenal, iliyomaliza ukame wa miaka 22 kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu huu, inatajwa kuingia sokoni kwa kasi ili kukisuka kikosi chao kwa ajili ya changamoto za msimu ujao. Jina la staa wa Aston Villa, Morgan Rogers, limeibuka kuwa kipaumbele cha kocha Mikel Arteta.
Rogers, mwenye umri wa miaka 23, amekuwa na msimu bora wa kuvutia ambapo alisaidia Aston Villa kutwaa taji la Europa League na kufuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kiwango chake kimevutia macho ya mabingwa hao wa EPL, huku mwandishi wa habari za michezo, Ben Jacobs, akidai kuwa dili hilo linaweza kukamilika haraka.
Ujumbe wa Jacobs kuhusu mustakabali wa Rogers
Katika podcast ya Latte Firm, Jacobs alitoa ufafanuzi kuhusu mpango huo wa Arsenal kumnasa nyota huyo ambaye ana uwezo wa kucheza nafasi ya winga wa kushoto na kiungo mshambuliaji (namba 10).
“Mimi natarajia kumuona Morgan Rogers akijiunga na Arsenal. Yeye ndiye mlengwa mkuu wa Arsenal kwa nafasi ya winga wa kushoto au namba 10. Taarifa nilizo nazo ni kwamba Rogers hana upendeleo wowote kuhusu nafasi kati ya hizo mbili atakayocheza,” alisema Jacobs.
Jacobs aliongeza kuwa mazungumzo kati ya klabu hizo yanatarajiwa kuanzia katika ada ya pauni milioni 80. Hii ni kutokana na makubaliano yasiyo rasmi yaliyokuwepo wakati mchezaji huyo alipoongeza mkataba wake mwaka jana, ambapo Villa waliahidi kutomzuia iwapo ofa kubwa itakuja.
Changamoto za ada ya uhamisho
Ingawa ada ya kuanzia ni pauni milioni 80, kuna taarifa nyingine zinazopendekeza kuwa bei ya Rogers inaweza kupanda zaidi. Mwandishi Graeme Bailey amebainisha kuwa kutokana na mkataba wa muda mrefu wa mchezaji huyo kutokuwa na kipengele cha kuuzwa (release clause), Aston Villa wako katika nafasi nzuri ya kupanga bei yao wenyewe.
Inaripotiwa kuwa Villa wanajilinganisha na usajili wa Florian Wirtz, wakiamini kuwa thamani ya Rogers sokoni kwa sasa inazidi kupanda kutokana na umri wake na kiwango chake bora. Klabu hiyo ya Birmingham inaona kuwa Rogers ni miongoni mwa washambuliaji vijana bora duniani, jambo linaloweza kuifanya Arsenal kulazimika kutoa zaidi ya pauni milioni 100 ili kupata huduma yake.
Kwa sasa, mashabiki wa Arsenal wanabaki wakisubiri kuona kama uongozi wa klabu hiyo utafanikiwa kumleta nyota huyo Emirates ili kuendeleza ubabe wao msimu ujao.