Manchester United yajipanga kwa Aurelien Tchouameni, Matheus Fernandes kutoa maamuzi
United yajipanga kumsajili Tchouameni
Manchester United inaendelea na mchakato wa kusuka upya kikosi chao cha kiungo kuelekea msimu ujao wa 2026/27, huku jina la nyota wa Real Madrid, Aurelien Tchouameni, likiendelea kutawala vichwa vya habari. Baada ya kuondoka kwa Casemiro kama mchezaji huru, United inahitaji kuimarisha eneo hilo la katikati.
Taarifa za hivi punde kutoka kwa mwandishi Ben Jacobs zinaonyesha kuwa suala la maslahi binafsi halitakuwa kikwazo kwa United kama wataamua kuendelea na mazungumzo rasmi. Inasemekana kuwa klabu hiyo ipo tayari kumfanya kiungo huyo kuwa mmoja wa wachezaji wanaolipwa mshahara mkubwa zaidi klabuni hapo ili kumpata.
Awali, Fabrizio Romano alithibitisha kuwepo kwa hamu kutoka United, ingawa alisisitiza kuwa hali hiyo haimaanishi mchezaji huyo anaondoka Santiago Bernabeu moja kwa moja, kwani kila kitu kitategemea maamuzi ya Real Madrid na mipango ya kocha wao kuelekea msimu ujao.
Matheus Fernandes kutoa uamuzi ndani ya siku chache
Wakati sakata la Tchouameni likiendelea, Manchester United pia inafuatilia kwa karibu saini ya Matheus Fernandes kutoka West Ham. Hata hivyo, United sasa inakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Tottenham Hotspur ambayo imeonyesha nia ya dhati ya kumnasa kiungo huyo.
Fernandes, ambaye bei yake inaweza kufika hadi pauni milioni 85, kwa sasa yupo katika nafasi ya kufanya maamuzi magumu. Ben Jacobs amebainisha kuwa mchezaji huyo anatarajiwa kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu klabu anayotaka kujiunga nayo kabla ya mwezi huu kuisha.
“Matheus Fernandes anatarajiwa kuamua ni klabu ipi anayoitaka kabla ya mwezi huu kwisha, na uamuzi wake unaweza kuisaidia klabu hiyo kupunguza bei iliyowekwa na West Ham,” alifichua Jacobs.
Mipango ya United katika dirisha la usajili
Kufikia sasa, Manchester United tayari imefanikiwa kumsajili Ederson Silva kutoka Atalanta kwa ada ya takriban pauni milioni 38. Hata hivyo, uongozi wa United unaonekana kutotosheka na saini hiyo pekee, kwani wanalenga kuleta angalau viungo wengine wawili ili kukamilisha safu yao ya kati.
Pamoja na Tchouameni na Fernandes, klabu hiyo inahusishwa na orodha ndefu ya wachezaji wengine. Kipaumbele cha United ni kuhakikisha wanasuka kikosi imara kitakachoweza kushindana kikamilifu katika mashindano mbalimbali msimu ujao. Mashabiki wanasubiri kuona ni nani atakayefuata kujiunga na Old Trafford katika siku chache zijazo.