Eddie Howe aondoka Newcastle, Matthias Jaissle kupewa mikoba yazua utata
Mabadiliko makubwa St. James’ Park
Klabu ya Newcastle United imetikiswa na taarifa nzito baada ya kocha wao Eddie Howe kuachana na timu hiyo kufuatia makubaliano ya pande zote mbili. Taarifa hii imethibitishwa na mwandishi maarufu wa habari za usajili, Fabrizio Romano, ambaye amesema kuwa klabu hiyo tayari imeanza mchakato wa kusaka mrithi wake.
Katika mchakato huo, Matthias Jaissle, ambaye kwa sasa anainoa Al-Ahli ya Saudi Arabia, ametajwa kuwa ndiye chaguo namba moja na tayari mazungumzo yameshafika hatua nzuri ili kumleta kocha huyo mwenye umri wa miaka 38 klabuni hapo.
Mashaka kuhusu uwezo wa Jaissle
Licha ya mafanikio yake nchini Saudi Arabia, ikiwemo kutwaa taji la Saudi Super Cup na kushinda AFC Champions League Elite mwaka 2025 na 2026, si kila mtu anayeamini kuwa Jaissle ndiye mtu sahihi wa kuiongoza Newcastle.
Don Hutchison, mchezaji wa zamani wa Sunderland na shabiki wa Newcastle, ametoa onyo kali kuhusu uamuzi huu. Kupitia mitandao ya kijamii, Hutchison alielezea kusikitishwa kwake na kuondoka kwa Howe na kuhoji uwezo wa Jaissle kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu ya England.
“Matthias Jaissle hataweza kufurukuta. Huu ni hatua kubwa ya kurudi nyuma duniani. Hapa ndipo gari linapoweza kupoteza mwelekeo na Newcastle kuanza kubadilisha makocha watatu au wanne katika kipindi cha miaka michache ijayo,” alisema Hutchison.
Nyota wanatarajiwa kuondoka
Hutchison hakusita kuonyesha hofu yake juu ya hatima ya kikosi cha Newcastle. Anaamini kuwa mabadiliko haya ya kocha yanaweza kuwafanya baadhi ya nyota muhimu kuamua kuondoka klabuni hapo katika dirisha hili la usajili.
Kulingana na maoni yake, wachezaji kama Bruno Guimaraes, Lewis Hall, na Tino Livramento wanaweza kuwa kwenye hatari kubwa ya kuondoka. Tayari kumekuwa na tetesi zinazohusisha Bruno Guimaraes na Arsenal, huku Manchester United ikitajwa kumfuatilia kwa karibu Lewis Hall.
Mtindo wa uchezaji utabadilika?
Kuhusu aina ya soka la Jaissle, Hutchison anaamini kuwa kocha huyo anaweza kushindwa kuzoea utamaduni wa Newcastle ambao umekuwa ukitegemea nguvu, kasi na kuifanya timu kuwa ngumu kufungika, hasa wanapocheza nyumbani.
“Yeye atajaribu kucheza soka la kuvutia, lakini kwa maoni yangu, toleo bora la Newcastle ni lile la kuwa timu ngumu sana kucheza dhidi yake. Mashabiki wa Newcastle hupenda staili hiyo, na nadhani hiyo siyo staili yake,” aliongeza Hutchison.