Manchester United bado wanapambana kumsajili Ederson, dili halijafa rasmi
Sintofahamu ya usajili wa Ederson na Manchester United
Kumekuwa na taarifa kinzani kuhusu mustakabali wa kiungo wa Atalanta, Ederson, kuelekea kujiunga na Manchester United. Huku baadhi ya vyanzo vikidai kuwa dili hilo limefika tamati, uongozi wa Manchester United umetoa msimamo tofauti ukiashiria kuwa bado kuna matumaini ya kukamilisha usajili huo.
Siku ya Ijumaa, mwandishi Fabrizio Romano alitoa taarifa iliyoleta mshituko kwa mashabiki wa United, akidai kuwa dili hilo limefeli na kuvunjika rasmi baada ya klabu hiyo kubadilisha mipango yao. Hali hiyo ilichagizwa na madai ya kuwepo kwa wasiwasi kuhusu hali ya afya ya mchezaji huyo, jambo ambalo Atalanta wamelikanusha vikali.
Msimamo wa Manchester United
Licha ya taarifa hizo za kuvunjika kwa mazungumzo, vyanzo kutoka ndani ya Manchester United vimeiambia Sky Germany kuwa bado wanapambana kuhakikisha Ederson anavaa jezi ya klabu hiyo. Mwandishi Florian Plettenberg amesisitiza kuwa taarifa zinazodai dili hilo limekufa kwa asilimia 100 si za kweli.
“Manchester United bado wanapambana kufanikisha dili la Ederson. Kwa hatua hii, vyanzo vya Man Utd vinakanusha kuwa dili limekufa. Mchakato bado ni mgumu, lakini wanasisitiza kuwa bado inawezekana kukamilisha usajili na mambo hayajaisha bado. Saa za maamuzi zinakuja,” alisema Plettenberg.
Atalanta waendelea kusisitiza mchezaji yupo fiti
Kwa upande wao, Atalanta wamesimama kidete wakisisitiza kuwa Ederson yupo katika hali nzuri ya kiafya. Mwandishi Nicolo Schira amedokeza kuwa klabu hiyo ya Italia sasa inapanga kumpa mkataba mpya kiungo huyo wa Kibrazili wenye maboresho ya mshahara ili kumshawishi abaki, kwani wanaamini hana tatizo lolote la kiafya.
Wakati huo huo, taarifa kutoka TEAMtalk zinaeleza kuwa vyanzo vya karibu na Atalanta navyo vimesema havijapata taarifa rasmi kutoka Manchester United kuwa dili hilo limefutwa au limekamilika.
Nini kinafuata?
Wakati sakata la Ederson likiendelea, Manchester United wanaendelea na mipango yao mingine ya kusuka upya eneo lao la kiungo. Tayari imeripotiwa kuwa kiungo wa Chelsea, Andrey Santos, amefuzu vipimo vya afya na kusaini mkataba wake, jambo ambalo linatarajiwa kutangazwa rasmi muda wowote kuanzia sasa.
Mashabiki wa United sasa wanabaki wakisubiri kuona kama jitihada za viongozi wao za kupambania saini ya Ederson zitazaa matunda, au kama changamoto za vipimo vya afya zitaendelea kuwa kikwazo cha usajili huo.