Matheus Fernandes: Aweka bayana chaguo lake kati ya Man Utd na Tottenham
Hatima ya Matheus Fernandes kuzivutia vigogo wa Premier League
Kiungo chipukizi anayekipiga ndani ya klabu ya West Ham, Matheus Fernandes, amekuwa gumzo katika kipindi hiki cha dirisha la usajili huku klabu kubwa za Manchester United na Tottenham Hotspur zikipigana vikumbo kumsajili.
Licha ya West Ham kushuka daraja msimu uliopita, kiwango cha mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 kiliwashawishi wadau wengi wa soka kuwa anastahili kucheza katika ngazi ya juu zaidi. Manchester United, ambao wako kwenye msako wa viungo wapya watatu, wamekuwa wakihusishwa kwa karibu na nyota huyo, hata hivyo, Tottenham nao wamejipanga kumpiku United ili kupata saini yake.
Chaguo la mchezaji na msimamo wa United
Ripoti za awali zilidai kuwa Matheus angetamani kutua Tottenham, lakini mwandishi nguli Andy Mitten ana mtazamo tofauti. Kupitia podcast ya ‘Talk of the Devils’, Mitten amesisitiza kuwa mchezaji huyo anapendelea kujiunga na Old Trafford kuliko kwenda London kaskazini.
“Manchester United wanaelewa kuwa mchezaji anataka kujiunga na klabu hiyo. Nimeambiwa angeweza kucheza Spurs, lakini anapendelea Manchester United,” alisema Mitten.
Changamoto kubwa inayokwamisha dili hili ni msimamo wa West Ham ambao wanataka kuvuna kiasi kikubwa cha pesa. Mitten anaongeza kuwa United hawataki kuingia kwenye ‘mnada’ wa kupandisha bei, huku wakala wa mchezaji huyo, Jorge Mendes, akitajwa kuwa na ushawishi mkubwa katika mchakato huu.
Bei ya £80 milioni yazua mjadala
Habari zinaeleza kuwa West Ham wanahitaji kiasi cha takriban £80 milioni ili kumwachia kiungo huyo. Bei hii imezua mjadala mkali, huku gwiji wa zamani wa Manchester United, Paul Ince, akielezea kushangazwa kwake na thamani hiyo.
Ince anahoji uhalali wa kiasi hicho kwa mchezaji ambaye amepata majanga ya kushuka daraja na timu zake mbili tofauti katika misimu ya hivi karibuni. “Kuhusu Matheus Fernandes kule West Ham… wanazungumzia £80 milioni. Kwangu mimi ni kitu cha ajabu. Kabla hajajiunga na West Ham, alikuwa na Southampton ambayo ilishuka daraja; sasa ana mfululizo wa kushuka daraja mara mbili, kwa hivyo kutaka kiasi hicho cha pesa ni kitu cha ajabu,” alisema Ince.
Ince aliongeza kuwa katika soka la kisasa, kiasi kikubwa cha pesa kama hicho kingepaswa kulipwa kwa mshambuliaji mwenye uhakika wa kufunga mabao 30 kila msimu, si kiungo pekee.
Kwa sasa, uamuzi unabaki mikononi mwa Manchester United ikiwa wako tayari kukidhi matakwa ya West Ham ili kumnasa mchezaji huyo ambaye anaonekana kuwa na nia ya kutua Old Trafford.