Thierry Henry aishauri Arsenal kutowauza Gyokeres kwa Alvarez
Henry ataka ushirikiano badala ya kubadilishana
Gwiji wa klabu ya Arsenal, Thierry Henry, ametoa ushauri mzito kwa uongozi wa ‘The Gunners’ kuhusu tetesi zinazoiunganisha klabu hiyo na mpango wa kubadilishana mshambuliaji Viktor Gyokeres ili kumnasa Julian Alvarez kutoka Atletico Madrid.
Ripoti mbalimbali barani Ulaya zinaashiria kuwa Atletico Madrid wako tayari kumuachia Alvarez ikiwa Arsenal wataweka mezani kiasi cha pauni milioni 50 pamoja na kumtoa Gyokeres kama sehemu ya dili hilo. Hata hivyo, Henry anaamini kuwa hii si hatua sahihi kwa timu inayotaka kujenga ufalme wa kudumu.
Utofauti wa wachezaji hawa
Katika maoni yake, Henry alisisitiza kuwa Julian Alvarez ni mmoja wa washambuliaji bora zaidi duniani kwa sasa, akionyesha uwezo wa kushinikiza, kutengeneza nafasi, kufunga, na kucheza katika maeneo tofauti ya uwanja.
“Alvarez ni mmoja wa washambuliaji waliokamilika zaidi duniani kwa sasa. Anaweza kushinikiza, kutengeneza nafasi, kufunga, na kucheza kati ya mistari. Lakini soka halichezwi kwenye karatasi. Gyokeres anaiipa Arsenal kitu kingine tofauti—nguvu, uwepo, na uchokozi mbele ya lango. Ni aina ya mshambuliaji ambaye mabeki wanachukia kukabiliana naye,” alisema Henry.
”Ubora juu ya ubora”
Henry alionya dhidi ya kubadilisha utambulisho wa kikosi cha Mikel Arteta kwa kutoa mchezaji ambaye tayari ameleta tija. Badala ya kufikiria kubadilishana, Henry anaona kuwa ndoto ya kweli ya Arsenal ingekuwa kuwa na wote wawili kwenye kikosi kimoja.
“Kama ningekuwa Arteta, ningetafakari sana kabla ya kumruhusu Gyokeres kuondoka, hata kwa ajili ya mchezaji mwenye kipaji cha pekee kama Alvarez. Timu kubwa hazibadilishi ubora kwa ubora tu; wakati mwingine zinaongeza ubora juu ya ubora. Hivyo ndivyo timu zinavyoweza kutawala ligi kwa muda mrefu,” aliongeza gwiji huyo.
Kwa sasa, uongozi wa Arsenal unakabiliwa na kazi ngumu ya kusawazisha bajeti na mahitaji ya kiufundi. Ikiwa watafanikiwa kuleta nyota wote wawili bila kuvuruga muundo wa timu, inaweza kuwa ni ishara ya wazi ya dhamira yao ya kutwaa mataji makubwa zaidi msimu ujao.