Tottenham kumsafirisha Mikey Moore kuelekea Ujerumani, dili la Gakpo kuwa gumu
Mikey Moore kujiunga na Koln kwa mkopo
Klabu ya Tottenham Hotspur inaonekana kuelekea kufunga dili la kumtoa kwa mkopo mchezaji wao kijana, Mikey Moore, ili aende kukuza kipaji chake katika klabu ya Koln nchini Ujerumani. Habari kutoka nchini Ujerumani, kupitia gazeti la Bild, zinasema kuwa mazungumzo hayo yako katika hatua za mwisho kukamilika.
Moore, mwenye umri wa miaka 18, msimu uliopita alikuwa kwenye mkopo katika klabu ya Rangers. Safari hii, Koln wameonekana kuvutiwa sana na kinda huyo na wanaamini atakuwa na mchango wa haraka katika kikosi chao kwa msimu ujao. Inafahamika kuwa ingawa awali Koln walitaka kuweka kipengele cha kumnunua moja kwa moja (buy option), Tottenham wamegoma na badala yake wamekubaliana kutoa mkopo wa msimu mzima bila kipengele hicho.
Safari ya Cody Gakpo ni ‘kazi bure’
Wakati Moore akielekea Ujerumani, uongozi wa Tottenham bado unaendelea na juhudi za kutafuta mshambuliaji mwingine, huku jina la staa wa Liverpool, Cody Gakpo, likitajwa sana. Hata hivyo, mchambuzi wa mambo ya soka, Ben Jacobs, ametoa onyo kali kuhusu dili hili.
Akizungumza kupitia kituo cha redio cha talkSPORT, Jacobs ameweka wazi kuwa kwa sasa, kujaribu kumng’oa Gakpo kutoka Anfield ni kazi ambayo haina tija kwa Spurs.
“Kwa sasa, vyanzo vimeeleza kuwa ni ‘kazi bure’ (fool’s errand) kwa Tottenham kujaribu kufanya mazungumzo na Liverpool kuhusu Gakpo. Liverpool hawapo tayari kumwachia hadi pale watakapofanikiwa kupata mchezaji mmoja au wawili wa kuziba nafasi yake,” alisema Jacobs.
Jacobs aliongeza kuwa kipaumbele cha Liverpool ni kuimarisha safu yao ya ushambuliaji kwanza, huku wakimtaka Bradley Barcola kama shabaha yao kuu. Hivyo, msimamo wa Liverpool hauwezi kubadilika hadi pale watakapokuwa na uhakika wa wachezaji wapya kuingia kikosini.
Tottenham wakiwa na msimu wa usajili mzito
Msimu huu wa usajili umekuwa na pilikapilika nyingi kwa Tottenham. Klabu imefanya uwekezaji mkubwa kwa kuleta nyuso sita mpya, ikiwemo wachezaji waliopatikana bure kama Marcos Senesi, Andy Robertson, na Martin Dubravka. Pia, wamewekeza kiasi cha pauni milioni 237 kumsajili Sandro Tonali, Mateus Fernandes, na Jan Paul van Hecke.
Baada ya kufanya usajili huo mkubwa, sasa klabu inaelekeza nguvu zake katika kupunguza idadi ya wachezaji wasiokuwa na nafasi, huku pia wakijaribu kuongeza washambuliaji wawili au watatu zaidi ili kukamilisha kikosi chao. Mbali na Gakpo, Spurs pia inahusishwa na mipango ya kumsajili Savinho, ingawa dili hilo linaonekana kutegemea maamuzi ya Manchester City kuhusu mbadala wake.