Arsenal yajipanga tena kumsaka Bruno Guimaraes baada ya ofa ya kwanza kugonga mwamba
Arsenal yatikisa mitaa ya St James’ Park
Klabu ya Arsenal inaonekana kuwa na dhamira ya dhati ya kuimarisha safu yao ya kiungo kuelekea msimu ujao, huku kiungo nyota wa Newcastle United, Bruno Guimaraes, akiwa ndiye mlengwa mkuu. Taarifa kutoka Uingereza zinathibitisha kuwa The Gunners wameanza mazungumzo rasmi kwa ajili ya kumnasa staa huyo wa Kibrazili.
Hata hivyo, jaribio la kwanza la Arsenal halijazaa matunda. Inasemekana kuwa klabu hiyo iliwasilisha ofa ya Pauni milioni 55, lakini uongozi wa Newcastle United umegoma kuachia kiungo huyo kwa kiasi hicho cha pesa. Newcastle inaonekana kutokuwa na haraka ya kumuuza nyota huyo, jambo linaloifanya Arsenal kutakiwa kurekebisha mkakati wao.
Ujumbe wa Fabrizio Romano
Mchambuzi wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, amethibitisha kuwa Arsenal walifikia hatua ya kuwasiliana na pande zote mbili; mchezaji mwenyewe na klabu ya Newcastle. Kulingana na Romano, Newcastle imefunga milango kwa ofa hiyo ya awali.
“Ni kweli kwamba Arsenal walifanya jaribio kwa Bruno Guimaraes. Walimfuata mchezaji na pia walifika kwa Newcastle. Uelewa wangu ni kwamba walitaka kufanya dili la takriban Pauni milioni 55, lakini Newcastle hawako tayari kumuuza kwa bei hiyo,” alisema Romano kupitia chaneli yake ya YouTube.
Romano ameongeza kuwa kwa sasa Guimaraes hana shinikizo la kuondoka na anaamua kuziacha klabu hizo mbili zimalizane wenyewe, huku akionyesha heshima kubwa kwa klabu yake ya Newcastle.
Safari ya Arsenal haijaishia hapo
Licha ya kukataliwa kwa ofa ya kwanza, vyanzo mbalimbali nchini Brazil vinadai kuwa Arsenal haijakata tamaa na inatarajiwa kurejea tena na ofa iliyoboreshwa. Kocha Mikel Arteta anatafuta kiungo wa kati mwenye ubora wa juu ili kuendelea kuimarisha kikosi chake kilichotwaa ubingwa wa Premier League.
Sambamba na harakati za Guimaraes, Arsenal pia inahusishwa na kinda wa Leicester City, Jeremy Monga. Ingawa ofa ya kwanza ya kumnasa kinda huyo ilikataliwa, kuna matumaini makubwa ndani ya kambi ya Washika Bunduki hao kuwa makubaliano yatafikiwa hivi karibuni ili kuepuka kesi za kisheria katika mahakama za soka. Monga mwenyewe anasemekana kuvutiwa na wazo la kujiunga na mabingwa hao watetezi wa ligi kuu ya England.